May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani walalamika wazee kufuata huduma mbali

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbarali

BARAZA la Madiwani halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameagiza serikali kuwarahisishia wazee wasiojiweza namna ya kupokea fedha za TASAF kwani mfumo uliopo kwa sasa kulingana na jiografia ya Mbarali inawalazimu kutembea kilometa zaidi ya saba kufuata huduma hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo,Novemba 13,2023 ,Diwani wa vitimaalum kata ya Ilongo ,Safihamidu Almasi katika kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani wa halmashauri ya Mbarali kilichofanyika katika ofisi za mkuu wa wilaya ya Mbarali ambapo amesema kuwa serikali imeendelea kutoa huduma kwa wananchi wenye hali ya chini kimaisha ambao wamekuwa wakinufaika na mfuko wa maendeleo ya jamii (TASAF).

“Ni kweli fedha hizi zimeingia katika halomashauri yetu ya Mbarali kwa robo ya kwanza lakini kumekuwepo na mabadiliko ya utaratibu wa namna gani mnufaika anaweza kuzipata fedha ikiwemo huyu mnufaika fedha zake kuingia kwenye akaunti yake benki lakini kwa hili naamini serikali ilikuwa na nia njema lakini imeleta changamoto kubwa kwani huduma hii wengi wao ni wazee na wananchi ambao wapo vijiji vya ndani ambavyo hata huduma za kibenki hamna hivyo wamekuwa wakitembea zaidi ya kilometa saba kwa ajili ya kufuatilia huduma hiyo ili waweze kutoa fedha zao na wengi wao ni wazee”amesema .

Pia Diwani huyo ameomba idara husika kufanya marekebisho madogo kuangalia ni wanufaika gani wenye kiwango gani ambao wanaweza kukabiliana na changamoto hiyo ,lakini pia waangalie umri kwa wazee ambao hawezi kutembea kutembea kilometa zaidi ya saba imekuwa ni mateso kwa wazee .

Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mbarali ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jeremia Kisangai ameiomba serikali kuwafikilia wazee hawa kwa kuwarudisha katika mfumo wa zamani wa upokeaji fedha ili kuweza kuwaondolea adha hiyo ya kuteseka kwa kutembea umbali mrefu.

Roman Kessy Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wilaya ya Mbarali amesema maboresho ya mfumo yanaendelea kufanyika kutokana na hitaji la mlengwa.

Amesema serikali imejitahidi kupunguza gharama na kuhakikisha wazee wanapata fedha kwa wakati lakini kulikuwa na uingizaji wa fedha taslimu, kwenye simu pamoja na benki na kwenye maeneo yenye shida kuna sehemu wanabadilisha wanaenda kwenye mfumo ambao wanaona ni rahisi kupatiwa huduma hiyo.

“Maboresho yanaendelea kufanyika kulingana na hitaji la mlengwa na mwisho kufika hatima na wengine kuishia benki au kupokelea kwenye simu lakini tunaamini changamoto hii itakwisha yote kulingana na maboresho yanayoendelea”amesema Kessy.

Katika hatua nyingine madiwani wamekubaliana kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara namna ya matumizi ya mfumo mpya wa ukusanyaji mapato TAUSI ili kuongeza mapato ya hamashauri.