July 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

BRELA yarahisisha usajili wa haki ya dhamana Kidijitali

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umeboresha huduma za usajili wa haki ya dhamana inayowekwa juu ya mali za kampuni (Charges), hatua inayowawezesha wadau kuwasilisha maombi yao kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika katika ofisi za wakala huo.

Hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya mfumo wa BRELA Online Service (BOS), unaolenga kuongeza ufanisi, kupunguza muda wa utoaji wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma za usajili kwa kampuni, taasisi za kifedha, ofisi za wanasheria na wadau wengine.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na BRELA, huduma hiyo ambayo awali ilihitaji wateja kufika ofisini, sasa inapatikana kikamilifu kupitia mfumo wa BOS ambapo nyaraka zote zinazohusu usajili wa haki ya dhamana zinaweza kuwasilishwa kwa njia ya kidijitali.

BRELA imeeleza kuwa waombaji wanapaswa kwanza kufungua akaunti kwenye mfumo wa BOS, kisha kuchagua huduma za kampuni (Company Services) na kuingia kwenye sehemu ya huduma za dhamana (Charges Services).

Baada ya hapo, watachagua huduma ya usajili wa dhamana (Registration of Charges), kubonyeza kipengele cha Register New Charges, kuingiza namba ya usajili wa kampuni husika na kukamilisha hatua zinazofuata, ikiwemo kujaza Fomu Na. 99 inayopatikana kupitia tovuti ya BRELA.

Aidha, BRELA imefafanua kuwa wateja ambao bado hawajafungua akaunti kwenye mfumo huo wanapaswa kutembelea mfumo wa BOS na kuchagua sehemu ya Create New Account, ambapo baada ya kujaza taarifa zinazohitajika watapokea maelekezo kupitia barua pepe yatakayowawezesha kuanza kutumia huduma hizo.

Wakala huo umehimiza wadau wote kutumia mfumo huo mpya wa kidijitali ili kunufaika na huduma za haraka, rahisi na zenye ufanisi zaidi.