Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Wadau wa Vyombo vya Uchunguzi kutoka Taasisi za Serikali wameshiriki mafunzo ya siku moja kuhusu Utekelezaji wa Kanuni za Wamiliki Manufaa.
Mkurugenzi wa Leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) Bw. Andrew Mkapa akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, leo tarehe 25 Novemba, 2022 jijini Dar es Salaam.
Amesema lengo la mafunzo hayo ni kujengeana uwezo kwa kiutendaji kama wadau na kushirikiana kwenye shughuli mbalimbali za kiutendaji kazi ikiwa ni pamoja na kufanya maboresho mbalimbali ya kisheria na kimfumo kwa niaba ya Serikali na kuhakikisha kunakuwa na utoaji wa huduma bora kwa umma.
“Lengo ni kukusanya maoni na ushauri kwa ajili ya maboresho zaidi ya utekelezaji wa Kanuni za Wamiliki Manufaa ili kuboresha utendaji kazi wetu wa kila siku pamoja na kuhakikisha kuwa vyombo vyote vya Uchunguzi vinapata taarifa zenye uhakika na kwa wakati,” amefafanua Bw. Mkapa.
Bw. Mkapa amesema kampuni zina umuhimu mkubwa katika kuchangia uchumi wa nchi, hata hivyo uzoefu unaonesha kwamba baadhi ya kampuni hutumika vibaya kwa kufanya vitendo vya kihalifu visivyokubalika kwenye jamii ikiwa ni pamoja na utakatishaji wa fedha haramu, kufadhili vitendo vya ugaidi, vitendo vya rushwa na hata ukwepaji wa kodi.
Bw. Mkapa amesema, Benki ya Dunia na Taasisi nyingine za Kimataifa zinazojihusisha na masuala ya kusaidia biashara zimejitolea kuleta mabadiliko ya hali hiyo kwa kuanzisha dhana ya Mmiliki Manufaa (Beneficial Ownership Concept) ambayo imeungwa mkono na Jumuiya ya Kimataifa ikiwemo Tanzania.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best