April 30, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Boti ya uvuvi yazama Dar, tisa wanusurika

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

BOTI ya uvuvi MV LEGACY yenye namba ya usajili DS/L1175 imezama ikiwa na watu tisa miongoni mwao wavuvi sita, mhandisi mitambo mmoja na manahodha wawili.

Watu wote tisa wamefanikiwa kuokolewa na wanaendelea vizuri kiafya bila ya kuwa na changamoto yoyote.

Kuzama kwa boti hiyo mali ya Yakoub Khamis, kumethibitishwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari leo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa; “Machi 10, 2024 10:1 alasiri, kituo chetu cha kuratibu shughuli za utafutaji na uokoaji (MRCC) kilipokea taarifa ya kuzama kwa boti ya uvuvi “MV LEGACY” iliyotokea saa 9:50 jioni karibu na fukwe ya Coco Beach, Msasani, Wilaya ya Kinondoni mjini Dar es Salaam.”

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kituo cha MRCC kilifanya jukumu lake la kisheria la kuratibu shughuli ya uokoaji kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi (Wanamaji) na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na kufanya juhudi za kufika eneo la tukio na kufanya zoezi la uokoaji.

Boti hiyo ambayo ilikuwa katika majaribio ya kiufundi baada ya matengenezo ya mifumo ya uvuaji samaki kwa kukokota (Trawling), ilianza majaribio majira ya saa 3:00 asubuhi ikitokea maeneo ya Tandavamba, Kivukoni na kufanya majaribio ya kuvua samaki wakizunguka katika maeneo yenye maji mafupi karibu na eneo la daraja jipya la Tanzanite (Upanga) hadi Coco Beach (Oysterbay).

“Ilipofika saa 9:50 Alasiri wakati nahodha alibadilisha uelekeo wa boti kuelekea upande wa kulia ndipo kamba moja ya upande wa kushoto ilikatika na kusababisha uzito kelemea kwenye kamba ya upande wa kulia na ndipo uzito ulipohama ghafla na kuilazimisha boti kunywa maji upande wa kulia kisha kuzama,” imeeleza taarifa hiyo na kuongeza;

“TASAC inaendelea kutoa rai kwa wamiliki na waendeshaji wa vyombo majini kuzingatia Sheria na Kanuni za udhibiti usafiri majini na kuhakikisha muda wote wanavalia majaketi okozi ili kujiepusha na maafa yanayoweza kusababishwa na tukio la ajali.”

Boti hiyo ilikuwa na urefu wa mita 11 na upana wa mita 1.7 ambapo ilipatiwa Cheti cha Usajili na Ubora na TASAC kufanya shughuli za uvuvi Machi 6,2024