May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya TADB yafunda wakulima matumizi ya kombaini havesta

Na Mwandishi wetu,TimesMajira,Online Mbarali

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Kilimo Tanzania (TADB), Ishmael Kasekwa, amewasihi wakulima wa mpunga wa Wilaya ya Mbarali kutumia kwa uangalifu mkubwa kobaini havesta 15 ambazo zimepokelewa wilayani humo kwa mkopo wa 950m/- kutoka TADB ili kulinda tunu ya uzuri wa mchele wao waliyopewa bure na Mungu na pia wanafuaike na tunu hiyo ndani na nje ya Tanzania.

Amewasihi wakulima kuelewa vizuri lengo la Serikali na TADB katika kufikisha zana bora za kilimo wilayani mwao.

Akizungumza hivi karibuni Kasekwa amesema shabaha ya Serikali nia ya dhati ya kukuza zao la mpunga, hasa katika Mkoa wa Mbeya kwa sababu mchele wa mkoa huo ni wadaraja la juu kabisa katika Afrika kutokana na ladha na harufu maridhawa ya mchele huo unapopikwa.

“Hii ni tunu ya Mungu kwenu na kwa Tanzania. Tumieni kombaini havesta hizi ili kuongeza tija katika kilimo cha mpunga hapa na kujiongezea faida.

Zana hizi hazikuja huku kwa kubahati mbaya, bali ni hatua ya makusudi ya benki yetu katika kukuza shabaha ya Serikali ya kuongeza kilimo cha mahindi na mpunga.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Ishmael Kasekwa akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Kilimo, Prof Adolf Mkenda (kushoto). Muda mfupi baada ya kukabidhi matrekta 15 yenye thamani ya sh. milioni 950 kwa Chama cha Msingi cha Nguvu Moja Wilayani Mbarali, Mbeya hivi karibuni. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine na wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Mbarali CCM (Picha na Mpiga Picha Wetu)

Mpunga wa hapa una sifa ya pekee katika jumuiya ya watafiti ndani ya Afrika na pengine dunia kote. Tumieni zana hizi kupunguza upotevu wakati wa mavuno na hasa ili mchele wenu ubaki ni kipenzi cha walaji ndani na nje ya Tanzania,” amesema huku akiwakumbusha wanachama wa Wanachama wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nguvu Kazi ya Wanavala waliopokea zana hizo.

Amesema chama hicho kimethibitisha kwamba mapinduzi katika kilimo cha mpunga yanawezekana kupatikana kwa ufanisi na kwa haraka wilayani Mbarali na mkoani Mbeya kama Serikali inavyotaka.

Zana hizo zimekabidhiwa hivi karibuni na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda. Wilaya ya Mbarali ina kaya 69,333, na kati ya hizo kaya 54,144 au asilimika 78.0 ni wakulima na asilimia 72.1 ya wananchi waishio vijijini ni wakulima, hasa wakulima wa mpunga.

Kulingana na sense ya 2012 Mkoa na Wilaya za Mkoa huo zinachukuliwa kuwa na wananchi waliosoma na wengi wao wakiwa na uelewa wa kutosha.
Asilimia 62.1 ya kaya 69,333 hizo ni wananchi wenye simu za kiganjani na asilimia 56.6 wanaweza kusafiri haraka kwa kutumia vyombo vya moto na baskeli.

Kasekwa amewaomba wananchi wa Mbarali kutumia mazingira mazuri yaliyopo kujiletea maendeleo kwa kuwa Serikali na benki yao inaunga mkono wakulima wanojituma.

“Macho yetu tumeyaelekeza kwenye mashamba yenu na zana mlizozipokea ili zitumike kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili kwa muda mrefu,” ameeleza mwenyekiti huyo ambaye ameteuliwa hivi karibuni na Rais Samia Hassan.

Akiizungumza wakati wa kukabidhi zana hizo, Mkurugenzi Mtandaji wa TADB, Japhet Justine, aliieleza hadhara hiyo kwamba tangu 2017 hadi mwezi huu benki imetoa zaidi ya sh. bilioni 12 za mikopo kwa wakulima kununua zana za kisasa za kilimo.

Kati ya hizo sh. bilioni 8.3 zimetolewa kununua zana za kisasa za kilimo 123: yaani matrekta 90, kombaini havesta zana 19, fedha iliyobaki ilinunua plau na zana za kupandia.

Amesema zana hizo zimenufaisha moja kwa moja wakulima 5800 katika mikoa ya Katavi, Manyara, Pwani, Kagera, Mwanza, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Tanga na wakulima wa Zanzibar.

Ameeleza pia kuwa sh. bilioni 3.7 zimetolewa kununua zana za kisasa za kilimo kupitia Mfuko wa Dhamana wa Wakulima Wadogo (SCGS), na kuwawezesha wakulima kupata jumla ya zana za kisasa 76. Alifafanua kwamba hatua hiyo imeifanya benki kufikia jumla ya uwekezaji katika zana za kisasa za kilimo kuwa sh. bilioni 12.

Alifafanua kuwa jumla ya mikopo ya sh. bilioni 13.9 imetolewa kama mikopo ya moja kwa moja na bilioni 9.4 imepitia mfukoa wa SCGS unaowawezesha wakulima na SME za kilimo kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi za fedha kwa udhamini wa TADB.