January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Afisa Masomo na Mauzo wa Bodi ya Nafaka na Mazao, Peter Mbole akitoa maelezo kwa mmoja wa wateja waliotembelea banda lao katika maonesho ya 44 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba.

Bodi ya Nafaka, Mazao yajipanga kwa masoko ya uhakika

Na Penina Malundo,Timesmajira Online, Dar es Salaam

BODI ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Tanzania (CPB), imesema imejipanga kuhakikisha kuwa na masoko ya uhakika kwa sababu bidhaa zao zimehakikiwa na kupata nembo ya ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Akizungumza kwenye viwanja vya maonesho ya 44, ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Afisa Masoko na Mauzo wa CPB, Peter Mobe amesema mradi huo ni mkubwa unaotarajia kuanza muda wowote pindi fedha zikipatikana na utakuwa mkombozi kwa wakulima.

Mobe amesema, katika mradi huo, ghala na vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi mazao mchanganyiko tani 520,000 kwa mara moja, litajengwa na kusaidia wakulima mbalimbali na hata mazao ya bodi hiyo kupata eneo la kuhifadhia lililo salama.

“Hili litakuwa ghala kubwa , litakuwa mkombozi kwa wakulima na hata sisi kwa sababu pia tunanunua mazao kutoka kwa wakulima na kuyahifadhi kabla ya kuongezea thamani kwa kusaga au kukoboa ili kupata unga bora na kuuza kwa bei nzuri zaidi, amesema Mobe.

Amesema, Dira ya CPB ni kuwa taasisi yenye mtandao mkubwa katika sekta ya nafaka na mazao mchanganyiko ifikapo mwaka 2025 na kwamba katika mradi huo wa ujenzi wa ghala kubwa, vinu sita vya kusaga nafaka navyo vitajengwa.

Mobe amesema, katika ujenzi huo vinu 46 vitajengwa, maghala 36 ambayo yote kwa pamoja yatakuwa na huo uwezo wa kuhifadhi tani 520,000 kwa wakati mmoja.

“Ni kweli moja ya kazi zetu, serikali iliidhinisha tufanye biashara ya nafaka na mazao nchanganyiko kama njia mojawapo ya kusaidia wakulima nchini kuwa na chombo cha uhakika kinachoweza kununua mazao yao kwa bei nzuri pia kuuza bidhaa za Tanzania zilizoongezwa thamani,”amesema Mobe.

Bidhaa zinazozalishwa na CPB ni pamoja na unga wa mahindi sembe na dona, korosho, maharagwe, mchele, mafuta ya alizeti na mazao mengine ya nafaka.

Akizungumzia jinsi wanavyozalisha bidhaa hizo Mobe amesema, wanaunua mazao bora kwa wakulima na kisha wanayachagua na kutoa uchafu wote kabla ya kupitia kwenye mashine kwa ajili ya hatua mbalimbali hadi kufikia kuzalisha unga.

“Tunanunua mazao kutoka kwa wakulima na tunayachagua yale salama na safi na kutolewa uchafu wote. Mfano mahindi baada ya kuyachagua yanapitishwa kwenye mashine kwenye eneo la kutoa chuma na kisha kulowekwa kwa muda maalum kutoa ganda na kutolewa alafu yanakaushwa na machine na kusagwa kutoa unga,”amesema Mobe.

Aidha, CPB pia ina uza mazao hayo nje ambapo miezi miwili iliyopita waliuza mahindi tani 5,000 nchini Rwanda, pia Jamhuri ya Demokrasia ya Congo(DRC), wameuza tani 500 za unga wa mahindi na Shirika la Kimataifa la Chakula Duniani (WFP),walinunua maharage tani 5,000 na mahindi tani 6,000.