July 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi ya Mkonge yahamasisha uwekezaji zao la Mkonge

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

Bodi ya Mkonge Tanzania imesema inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika mnyororo mzima wa thamani wa zao la mkonge ili kuongeza tija, ajira na mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kwa upande wake Afisa Masoko wa Bodi ya Mkonge Tanzania, Best Rukanda, amesema wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) kuwa mkonge ni zao lenye fursa nyingi za kiuchumi kuanzia kilimo, uchakataji viwandani, utengenezaji wa bidhaa mbalimbali hadi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Amesema bodi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na wawekezaji kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya mkonge, ikiwemo uwekezaji katika mashamba, viwanda vya uchakataji, utengenezaji wa mashine pamoja na uzalishaji wa mbegu kupitia vitalu maalum.

“Tunazungumzia mnyororo mzima wa thamani wa mkonge kuanzia uzalishaji wa malighafi, uchakataji, utengenezaji wa bidhaa na usafirishaji wa bidhaa hizo kwenda masoko ya kimataifa. Kuna fursa nyingi ambazo bado hazijatumika kikamilifu,” amesema Rukanda.

Alieleza kuwa mkonge hutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo kamba, vikapu, mikeka, kapeti na bidhaa nyingine zinazotokana na nyuzi zake, huku mahitaji ya bidhaa hizo yakiendelea kuongezeka katika masoko ya kimataifa.

Aidha, amesema mkonge una matumizi mbadala yanayozidi kufungua milango ya uwekezaji, ambapo nyuzi zake hutumika kutengeneza kamba maalumu zinazotumika katika mashine za lifti, huku mabaki ya zao hilo yakitumika katika uzalishaji wa chakula cha mifugo na bidhaa nyingine za viwandani.

Kwa mujibu wa Rukanda, tafiti na maendeleo ya teknolojia yameendelea kubaini matumizi mapya ya mkonge, jambo linaloongeza thamani ya zao hilo na kuvutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Ametoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa zilizopo katika tasnia ya mkonge kwa kuwekeza katika maeneo mbalimbali ya uzalishaji na uchakataji ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuchochea maendeleo ya viwanda nchini.

Pia amewahamasisha Watanzania kutembelea banda la Bodi ya Mkonge katika maonesho mbalimbali ya biashara ili kupata elimu kuhusu zao hilo, matumizi yake na fursa za uwekezaji zinazopatikana katika sekta hiyo.“Tunakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza katika tasnia ya mkonge kwa sababu bado kuna fursa nyingi ambazo hazijatumika kikamilifu na zinaweza kuleta manufaa makubwa kwa uchumi wa taifa,” amesema.