November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodi wapongeza utendaji wa TANESCO

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BODI ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO ) ikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi Dkt. Alexander Kyaruzi wameipongeza TANESCO kwa kasi kubwa ya utekelezaji na uendelezaji wa huduma za umeme wa uhakika kuendana na kasi kubwa ya ukuaji wa Jiji la Dodoma kwa sasa.

Dkt. Kyaruzi ameeleza kuwa kituo cha kupoza na kusambaza Umeme cha Zuzu Dodoma, kina uwezo wa Megawati 48 ambapo kwa sasa zinatumika Megawati 35 kulingana na matumizi yaliyopo, ziada ikiwa ni Megawati 13 kwa Dodoma lakini pia zitaongezwa tena Megawati 250.

Amesema,
TANESCO tayari wanakamilisha upanuzi wa kituo cha Zuzu, upanuzi ambao utaongeza Megawati hizo 250 za ziada, hivyo kuwezesha upatikanaji wa takriban Megawati 300 kwa Jiji la Dodoma kuendana na kasi ya ukuaji wa Jijini hilo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco Dkt. Alexander Kyaruzi (kushoto anayezungumza) akiwa na wajumbe wa bodi ya Tanesco wakifanya ukaguzi wa miundombinu ya umeme jijini Dodoma.

Dkt. Kyaruzi ameongeza kuwa, kasi ya Jiji la Dodoma kupanuka kwa ujenzi wa makazi mapya, uwekezaji mpya, huduma za kijamii, ukuaji wa uwekezaji katika biashara pamoja na viwanda ni mkubwa hivyo kufanya mahitaji ya umeme kuongezeka kwa kasi kila siku.

“Tumeridhishwa na kasi ya TANESCO baada ya kujionea kuwa wanakaribia kukamilisha upanuzi wa kituo cha Zuzu kwa kuongeza tranfoma mbili kubwa zitakazo ongeza Megawati 250 za ziada. Ongezeko hilo litawezesha upatikanaji wa umeme mwingi na uwekezaji mkubwa Jijini Dodoma,” amesema Dkt. Kyaruzi.

Dkt. Kyaruzi ameongeza kuwa ndani ya mwezi Septemba upanuzi huo utakuwa umekamilika na umeme huo utakuwa tayari kwa matumizi kulingana na mahitaji yote Jijini Dodoma.

Kwa upande wa Msimamizi wa mradi huo Mhandisi Peter kigadye ameeleza kuwa, TANESCO inatekeleza miradi mikubwa ya umeme kwa ustadi mkubwa ikitumia uzoefu ilioupata katika upanuzi na uendelezaji wa miundombinu ya umeme katika majiji ya Dar es Salaama, Mwanza na Arusha.