May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodadoba Combine yawaandalia dozi Bodaboda Mtwara

Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online, Bukoba

TIMU ya soka ya Bodaboda ya Mkoa wa Kagera ‘Bodaboda Combine’ inatarajia kuchuana vikali na timu ya Bodaboda ya Mkoani Mtwara katika mchezo wa kirafiki utakaochezwa Desemba 12 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku wakitamba kuwashushia kichapo kikali wapinzani wao.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika uwanja wa Kaitaba, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amesema kuwa, timu hiyo ya Bodaboda Mkoa imetokana na Ligi ya JPM Cup iliyofanyika miezi miwili iliyopita iliyoshirikisha timu kutoka kila Kata huku timu hiyo ikiibuka na ubingwa.

Mkoa uliamua kuanzisha JPM Bodaboda Cup iliyokuwa na lengo la kuwaweka vijana pamoja na kuwajengea weledi na uwezo katika suala zima la kushirikiana na vyombo vya dola kuimarisha Usalama wa Ulinzi na Usalama Barabarani.

Pia mashindano hayo yalitumika kuunda vikundi mbalimbali vya bodadoba ili kuwainua kiuchumi kupitia vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitawafanya waweze kupata kipato nje ya kazi ya bodaboda.

Amesema, tayari timu hiyo ilishaanza maandalizi yake toka desemba 5 na wanaendelea vizruri na maandalizi yao kwani mikakati yao ni kuhakikisha wanafanya vizuri na kuibuka washindi wa mchezo huo.

Brigedia Jenerali Gaguti amesema, timu hiyo itakapokuwa Dar, wachezaji watapata fursa ya kutembelea miradi mitatu mikubwa ya miundombinu inauosimamiwa na serikali.

“Kwa sasa timu yetu inaendelea na mazoezi kuelekea kwenye mchezo dhidi ya timu ya bodaboda kutoka Mtwara ambao tunahitaji kupata ushindi. pia niwaombe wananchi na wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono timu yetu kwani kwa sasa suala la michezo lazima lipewe kipaumbele kwani imekuwa ikichangia kutoa ajira kwa vijana,” amesema kiongozi huyo.

Kocha mkuu wa timu hiyo ya bodaboda Combine, Kengera Mayunga alisema, toka timu hiyo imeingia kambini hadi sasa wachezaji wanaendelea kuimarika na anaimani kubwa kuwa watapata ushindi dhidi ya wapinzania wao.

“Mkuu wa Mkoa ametoa ushirikiano wa kutosha kwa vijana ili waweze kuendekeza vipaji vyao na sisi hatutamuangusha katika mchezo huu kwani tunatambua kuwa tunakwenda kukutana na timu yenye wachezaji wazuri lakini ni lazima tupambane kupata ushindi ili kutangaza pia wachezaji wetu,”.