May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodaboda waelimishwa juu ya vitendo vya ukatili

Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online, Mwanza

Katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, elimu imeendelea kutolewa kwa makundi mbalimbali ikiwemo waendesha bodaboda,ambao wito umetolewa kwao kuacha tabia ya kuwafanyia vitendo vya ukatili wanawake na watoto.

Ambapo siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uadhimishwa kila ifikapo Novemba 25 hadi Disemba 10, na kwa mwaka 2022 yakiambatana na kauli mbiu isemayo “Kila Uhai una Thamani: Tokomeza Mauaji na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isaack Ndasa, akizungumza wakati akifungua kongamano la waendesha bodaboda na bajaji mkoani hapa,ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii, amewataka kuacha tabia ya unyanyasaji na ukatili wanapokuwa wanawasafirisha abiria hususani watoto na wanawake ambao ndio wateja wao wakubwa.

“Kumbuka ukimtendea ukatili mtoto wa mwenzio, wa wako pia hatakuwa salama maana ukatili huo utakurudia kwani ndivyo imani ilivyo,kwani kuna baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji ambao wamekuwa wakiwafanyia wanafunzi na wanawake vitendo vya ukatili ikiwemo wa kingono ambao ni abiria wao wakati wakienda au kutoka kwenye shughuli zao,”ameeleza Ndasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za watoto na wanawake la KIVULINI, Yassin Ali, ameeleza kuwa kundi hilo la waendesha bodaboda limekuwa likichangia ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Hivyo kufuatia elimu inayotolewa kwa waendesha bodaboda na bajaji itasaidia kuwaweka salama watoto na wanawake.

Pia Yassin,ametoa wito kwa jamii kuzingatia malezi bora kwa watoto kwani takwimu za jeshi la polisi kuanzia mwezi Januari hadi Septemba zinaonesha jumla ya watoto 1,044,wamelawitiwa huku watoto wa kiume wakiwa waathirika zaidi kwa kuwa watoto 878 na wakike wakiwa ni 166.

Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa Mwanza, Dustan Kombe,amewataka bodaboda hao kuacha kuwatendea ukatili watoto ambao ni wateja wao hivyo uwaamini na kuwaagiza nyumbani kwao.

Huku akiwasihi bodaboda hao kutowaamini watu wasiowafahamu na kutowaachia bodaboda nyakati za usiku kwani hao ndio wanawaharibia sifa kwa kujihusisha na vitendo vya ukatili.

Sanjari na hayo amewahimiza waendesha bodaboda na bajaji kuzingatia elimu wanayopewa ili kuwa sehemu ya kuimarisha usalama katika jamii.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto kutoka Jeshi la Polisi Mkoa Mwanza, Faraja Mkinga, ameeleza kuwa unakuta bodaboda unamuamini, unamwagiza nyumbani kwako kila siku, unakuja kugundia amemgeuza mtoto wako kuwa mkewe hivyo aliwaonya kuachana na tabia hiyo kwani hawata ukwepwa mkono wa sheria.

Baadhi ya waendesha bodaboda na bajaji wa jijini Mwanza,akiwemo Mwenyekiti wa bodaboda Kanda ya Mwanza Mjini, Ramadhan Kakuba,amewataka waendesha bodaboda wenzie kutoa taarifa polisi au kwenye chama chao endapo atamuona mwenzie anayejihusisha na vitendo vya ukatili.

“Taarifa yako itakuwa siri, sheria itachukua mkondo wake, wale ambao hawajapa vitambulisho, wafike ofisini wasajili ili watambulike,”amesisitiza Kakuba.

Naye Paulo Bundala ameishauri jamii kubadilika na kuacha kuwatumia bodaboda wasio na vituo rasmi vya kazi kwani hao ndio wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani nyakati za usiku.

Baadhi ya bodaboda wa jijini Mwanza,wakiwa katika maandamo ya kuelekea kwenye kongamano la waendesha bodaboda na bajaji mkoani Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku 16 ya kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.
QOfisa Maendeleo ya Jamii Mkoa Mwanza, Isack Ndasa akizungumza wakati wa kongamano la bodaboda jijini Mwanza lenye lengo la kutoa elimu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.