January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bodaboda kujengewa vituo vya maegesho

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

Serikali kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa waendesha pikipiki za magurudumu mawili maarufu kama ‘bodaboda’ kwa kujengea vituo maalumu vitakavyotumika kwa ajili ya maegesho wakati wakisubiri abiria tofauti na ilivyo sasa.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema Halmashauri kwa kushirikiana na bodaboda wataangalia maeneo yanayofaa ili kuweza kujenga vituo vya maegesho watakavyotumia na siyo vijiwe kama wanavyoita sasa.

Mpogolo ameyasema hayo Machi 5, mwaka huu jijini Dar es Salaam,kwenye mkutano ulioandaliwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, ukihusisha dereva bodaboda 670 wa jimbo hilo wenye lengo la kusikiliza changamoto zao pamoja na kuelezea nia ya Serikali juu ya maboresho hayo.

Ambayo Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Ilala kwa kushirikiana na viongozi wa umoja wa bodaboda hao, kuhakikisha zinapatikana sehemu maalumu ambazo zitajengwa vituo hivyo.

Amesema kuwa maboresho hayo yatakuwa endelevu ambapo dereva bodaboda wote watalazimika kuvaa ‘Reflector’ ili waweze kutambulika kwa urahisi ikiwa ni pamoja na kukomesha vitendo vya kihalifu, ambavyo mara nyingi vimekuwa vikihuhusisha kundi hilo.

Pia Mpogolo, amewataka ‘bodaboda’ hao kujirasimisha ili wawe kwenye mfumo rasmi, ambao utawasaidia kuwa katika ajira rasmi lakini kuaminiwa na kukopesheka katika taasisi za kifedha hivyo kujikwamua kiuchumi.

Sanjari na hayo amewasisitiza kuwa na umoja na mshikamano huku akiwahimiza kujiunga katika vikundi kujiunga ili kuwarahisishia kupata mikopo inayotolewa na halmashauri.

Huku akidai kuwa, hadi sasa Halmashauri hiyo ina bilioni 7 ambazo hivi karibuni mikopo itaendelea kutolewa baada ya kusitishwa kwa muda mrefu kutokana na baadhi ya watu kutokuwa waaminifu wa kutorejesha.

Kwa upande wake Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, amewataka dereva bodaboda hao kuendelea kuwa wavumilivu na kudai kuwa mikopo ya asilimia 10 itarejea hivi karibuni na itatolewa kwa haki na usawa.

Nae,Ofisa Usafirishaji wa LATRA, Ashel Mwihambi, amewataka dereva bodaboda kukata leseni ya usafirishaji kwa maendeleo ya nchi.