May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Biteko ataka umeme ufike kwenye huduma za kijamii

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko, leo ameanza ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kagera ambapo katika siku ya kwanza ya ziara yake amewasha umeme katika Kijiji cha Mubaba na Nyantakara vilivyopo wilayani Biharamulo.

Akizungumza na wananchi pamoja na viongozi wa Serikali na wakandarasi wa umeme vijijini, Dkt.Biteko ameagiza kuwa, sehemu zinazotoa huduma za kijamii kama vile shule, visima vya maji na vituo vya afya zipewe kipaumbele katika kupelekewa umeme ili wananchi waweze kupata huduma bora.

“Haileti maana umeme kufika katika eneo fulani kama watoto wanasoma gizani, haileti maana umeme kufika hapa halafu kina mama
wanajifungulia gizani, wala haina maana umeme kufika hapa wakati kuna vyanzo vya maji na tunashindwa kuwapelekea maji watu wetu, ndio mana Rais wetu anataka mfikiwe na umeme ili usaidie kuboresha huduma na kuchagiza shughuli za uchumi,” Amesema Dkt.Biteko

Dkt.Biteko ametoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu ya umeme na wawakemee watu wanaoiba miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo, mafuta ya transfoma kwani wanarudisha nyuma jitihada za kuwafikishia umeme wa uhakika wananchi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Doto Biteko, (wa Nne kutoka kulia) akikata utepe kuashiria umeme kuwashwa katika Kijiji cha Mubaba wilayani Biharamulo mkoani Kagera. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa.

Kuhusu wakandarasi wanaosimamia miradi ya umeme amesema, wahakikishe wanafanya kazi kadri ya mikataba inavyoelekeza na kwamba
kama kuna changamoto zozote wazieleze kwa viongozi, lakini REA wakiona kuna mkandarasi ambaye hafanyi kazi kama inavyotakiwa, mkandarasi huyo aondolewe na awekwe mwenye uwezo.

Katika hatua nyingine, Dkt.Biteko amesema atasimamia ipasavyo agizo la Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan la kudhibiti changamoto ya
kukatika mara kwa mara kwa umeme ndani ya kipindi cha miezi sita.

“Agizo hili la Rais tutalisimamia na kuhakikisha shida hii tunayoiona ndani ya kipindi cha miezi tunaipunguza kwa kiasi kikubwa ili watanzania wapate umeme wa uhakika.”Amesema Biteko

Kuhusu nishati safi ya kupikia amesema, Serikali inakuja na mpango utakaowezesha wananchi kupunguza matumizi ya kuni na mkaa wa
asili ambao una athari kwa afya na kuleta nishati safi ambapo REA inakuja na mpango unaojumuisha kugawa mitungi ya gesi kwa wananchi kwani lengo la Serikali ni kuhama kutoka nishati isiyo safi na kwenda kwenye nishati safi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, (wa Pili kutoka kulia) akiwasha umeme katika moja ya nyumba katika Kijiji cha Nyantakara wilayani Biharamulo mkoani Kagera ikiwa ni ishara ya kuwasha umeme kwenye Kijiji hicho.