Na Nuru Mwasampeta, WM
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amewataka Watanzania kuutazama mchango wa sekta ya madini kwa namna unavyosaidia kuinua sekta nyingine za uchumi, kwani tayari kwa upande wa kuongezeka kwa ukusanyaji wa maduhuli sekta hiyo imeonesha mafanikio makubwa.
“Niliwaambia wenzangu wizarani, lazima tuhame sasa kwenye mfumo wa kufurahia kuona mapato yameongezeka kutokana na ukusanyaji wa maduhuli twende kwenye mfumo wa kujiuliza je? Sekta ya madini imechangiaje ukuaji wa sekta nyingine?.
“Anayelima mchele awe na uhakika wa wanunuzi kwa sababu wachimbaji wapo, anayefuga ng’ombe awe na uhakika wa soko kwa sababu wanunuzi wapo, anayelima nyanya na shughuli nyingine hivyo hivyo, na huo ndio tunaita ufungamanishaji wa uchumi wa madini na sekta nyingine;
Waziri Biteko amebainisha hayo hivi karibuni mkoani Geita alipofanya ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo inayofanywa kwa fedha za huduma za jamii (CSR) zinazotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) ambapo alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya unaoendelea katika soko kuu la dhahabu Geita pamoja na soko la Katundu litakalohusisha biashara za kawaida lililojengwa katika Halmashauri ya Mji wa Geita.
Pamoja na kukagua miradi ya maendeleo inayowezeshwa na GGML, Waziri Biteko amezungumza na wafanyabiashara wa madini mkoani humo na kueleza kuwa kutokana na changamoto ya Covid-19, wizara imetoa kipindi cha miezi mitatu kwa wafanyabiashara wa madini kununua madini mahali popote nchini na kuwataka kuzingatia uwepo wa vibali vyote muhimu vinavyoonesha mahali madini hayo yamenunuliwa na yanakopelekwa mara baada ya kuyanunua.
Akitoa taarifa ya sekta, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema mwenendo wa biashara ya madini ya dhahabu katika mkoa wake tangu soko la dhahbu kufunguliwa mwezi Machi 2019 hadi Mei 2020 kipindi cha miezi 14 jumla ya kilo 5,320.99 zenye thamani shilingi Bilioni 522.44 zimeuzwa na kuchangia mapato ya serikali kupitia mrabaha na ada ya ukaguzi kwa jumla ya shilingi bilioni 36.57.
Amesema, ongezeko hilo linaonesha namna sekta ya madini ilivyokuwa na mafanikio makubwa sana kutokana na usimamizi makini na uongozi bora wa wizara, lakini pia utii na utekelezaji wa ushauri na maelekezo yanayotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Aliongeza kuwa, fedha inayopatikana kutokana na makusanyo kwenye sekta ya madini ndiyo inayokwenda kulipa elimu bure, kujenga vituo vya afya, inatumika katika kujenga hospitali za wilaya na mambo mengine mengi yanayotekelezwa na serikali yetu.
Amebainisha kuwa, mkoani Geita kuna ongezeko kubwa la viwanda vya kuchenjua dhahabu (Illusion Plant) kutoka viwanda 20 vilivyokuwepo awali na kufikia viwanda 39 na kubainisha kuwa hayo ni mageuzi makubwa katika sekta ya madini kwa kuwezesha uwepo wa viwanda vidogovidogo mkoani humo.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best