January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bingwa mbio za magari amuangukia Rais Samia, Wizara

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

BINGWA wa Mbio za Magari Mkoani Tanga ‘Usambara Rally 2021’ Ashu Ramzan, amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mchezo huo.

Ramzani alitwaa ubingwa huo katika mashindano yalishirikisha washiriki 16 kutoka Mikoa mbalimbali  pamoja na wengine waliotoka nchi za jirani ikiwemo Kenya yakiendeshwa kwa kuchangiwa na wadau.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Ramzan amesema, kwa miaka ya hivi karibuni mchezo huo umekuwa miongoni mwa michezo inayopendwa zaidi na umekuwa kimbilio kwa vijana wengi kwani umekuwa ukitoa ajira kutokana na kwamba wanaposhiriki wanapata manufaa makubwa kwao na jamii inayowazunguka.

Ikiwa vijana watainuliwa zaidi katika upande huo basi wataweza kuitangaza nchi kimataifa kwani wanaonesha ushindani mkali katika mashindano ya ndani hivyo ikiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa atahamasisha wadau kuutupia jicho na mchezo basi waamini utalitangaza taifa vizuri kama ilivyo mchezo wa ngumi, riadha na mingine.

“Mchezo huu ni mzuri, unapendwa sana na vijana na umekuwa kimbilio lao kubwa hivyo tunaiomba Serikali inayoozwa na Mama Samia Suluhu Hassan pamoja na wadau waone namna nzuri ya kutoa sapoti kwenye mchezo huu ambao unatumiwa na vijana kama sehemu yao ya kujiingizia kipato,” amesema Ramzan.

Akizungumzia furaha yake baada ya kutwaa ubingwa huo, amesema ndoto kwa wakazi wa Tanga kabla ya kuanza mashindano hayo ilikuwa ni kuona anashinda na kweli alifanikiwa kubeba ubingwa katika mashindano yake hayo ya 10 ambapo alinza akiwa kama msoma ramani ‘Navigator’.

Kwa sasa matarajio yake kwenye mchezo huo ni kufika mbali zaidi na anaamini ikiwa changamoto ya udhamini pamoja na mambo mengine zikitatuliwa basi ushindano utakuwa mkubwa zaidi na kuweza kuiwakilisha nchi vizuri kimataifa.

“Ninaomba wadhamini kujitokeza kwa wingi, wapo ambao wameanza kujitokeza lengo kubwa likiwa ni kuhakikisha mchezo huu unapata mafanikio makubwa zaidi kwani maandalizi ya kuandaa gari la mashindano ni kubwa sana,” amesema Ramzan.