January 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bilioni 6 kutekeleza miradi Mbarali

Na Esther Macha, Timesmajira,Online, Mbarali

Imeleezwa kuwa katika kipindi cha mwezi Julai 2022 hadi Machi 31,mwaka huu zaidi ya bilioni 6,zimepokelewa jimboni Mbarali, kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Akizungumza na Majira Online,leo Aprili 23,2023 Mbunge wa Jimbo la Mbarali ,Francis Mtega amesema wamepokea kiasi hicho kwa ajili ya kuboresha miradi mbalimbali ikiwemo sekta ya elimu.

Mtega amesema kumekuwa na utekelezaji wa miradi mingi kulingana na fedha inayotolewa na serikali, ambapo mbali na sekta ya elimu pia wamepokea fedha kwa ajili ya kuboresha miradi ya miundombinu ya barabara za pembezoni ambazo zilisombwa na mafuriko.

Mbunge huyo amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023, pia wametenga zaidi ya bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara kupitia Mfuko wa Matengenezo ya Barabara,tozo ya mafuta, Mfuko Mkuu wa Serikali na fedha za maendeleo.

Aidha Mtega amesema hadi kufikia Machi 2023 jumla ya bilioni 2 sawa na asilimia 78 zilipolekewa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi mbalimbali ambao mpaka sasa zimefika asilimia 87.23.

“Ndugu zetu wa Tarura wamefanya kazi kubwa kilichokuja kukwamisha kwa mwaka huu ni kunyesha mvua kubwa ambazo zilisababisha mafuriko makubwaa ambayo yaliathiri baadhi ya barabara za Igurusi,Utengule,Ihahi,Mgolongolo,-Chang’ombe, Nyeregete na maeneo mengine,”amesema Mtega.

Hata hivyo amesema kuwa katika kuhakikisha miundombinu hiyo inafanyiwa marekebisho amewasiliana na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA)ili kuweza kufanya matengenezo ya dharura na kuwezesha wananchi kusafirisha mazao yao pamoja na shughuli zingine za kijamii kwa msimu huu kilimo.

Mkazi Igalako wilayani hapa Juma Shaban, amesema Mbunge wa Jimbo hilo amekuwa akijitahidi kutatua changamoto mbalimbali kila zinapotokea lakini kilichokuja kuleta shida ni mvua ambazo zilisababisha mafuriko makubwa ambayo yalisababisha miundombinu ya barabara kwa baadhi ya maeneo kuharibika.

Kwa upande wake Diwani viti Maalum Kata ya Igurusi ,Hawa Kihwele amesema kuwa uwakilishi wa Mbunge ,Francis Mtega bungeni kumeleta msukumo wa serikali kuongeza fedha za bajeti za miradi ya maendeleo.