May 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Stanbic, Kampuni ya Ramani zaingia makubaliano

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

BENKI ya Stanbic imeingia makubaliano na Kampuni ya Ramani kwa lengo la kuwafikia wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa mbalimbali  za viwandani kwa kuwapa mikopo na mitaji ya kuendeleza biashara zao.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam juzi wakati wa kusainiwa kwa makubaliano hayo mkurugenzi wa biashara wa Benki hiyo, Frederick Max, ameeleza kuwa makubaliano hayo yataiwezesha Benki hiyo kufikisha huduma za kibenki kwa wateja wengi zaidi.

Amesema Benki imeshatoa mikopo yenye thamani ya h. bilioni 50 kwa mwaka jana, ambapo kwa mwaka huu inataraja kutoa sh. bilioni 150 kwa ajili ya wasambazaji wa bidhaa za viwandani.

“Tumeingia makubaliano na Ramani ili kuweza kuwafikia wasambazaji wa bidhaa mbalimbali hii itatuwezesha sisi kufikisha huduma zetu za kibenki kwa wahitaji wengi zaidi kwa sababu Ramani tayari wana wateja wao nchi nzima na sisi tunaleta ujuzi wetu wa masuala ya kibiashara,”alisema na kuongeza;

“Sisi kama Benki tunajiskia fahari na faraja kuweza kuwa nao kuhakikisha wafanyabiashara wengi sana wanafaidika na huduma za kibenki.”

Alisema kwenye kiasi ambacho wametenga  kwa ajili ya uwezeshaji, tayari wametoa mikopo yenye thamani ya sh. Bilioni 50 kuanzia Desemba mwaka 2023 hadi sasa na mwaka huu wanatarajia kuongeza mkopo huo mara mbili.

Kuhusu mikopo chechefu katika Benki hiyo, Max alisema wapo chini ya asilimia 5 ambayo inaonekana ni mwamko wa kibiashara na fursa mbalimbali ambazo zinatokana na miradi mbalimbali ambayo imewekezwa nchini pamoja na Serikali ambayo imewezesha miradi na shughuli mbalimbali za kibiashara kufunguka.

Kwa upande wake Afisa Mkuu Mtendaji wa Ramani, Iain Usiri, alisema makubaliano hayo yataiwezesha Benki hiyo kuwafuatilia wateja wao kwa ukaribu zaidi, lakini pia yamelenga kufikisha ujumuishi wa huduma kifedha kwa Watanzania.

Pia alisema kampuni hiyo inawapa wauzaji programu ya teknolojia ya umiliki wa kifedha ili kurahisisha shughuli zao.

“Kwa hivyo tunazindua soko la fedha ili benki inayofanya kazi nasi kupitia teknolojia yetu iweze kupata data ya wakati halisi na tathmini za hatari za wauzaji wa FMCG,”alisema.

Afisa Mtendaji mkuu wa Ramani (Mkurugenzi Mtendaji), Iain Usiri, (wa kwanza kushoto) ,Mkurugenzi wa biashara wa Benki hiyo Frederick Max (wa kulia) wakikabidhiana mikataba waliosaini hapo Juzi wenye lengo la kukuza biashara kwa kuwezesha wasambazaji wa bidhaa za matumizi ya Kila siku ( Picha na Mpigapicha wetu)