May 18, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya Kilimo kuinua alizeti Singida kwa bilioni 8.2

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Singida

BENKI ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) imeshatoa Mikopo inayofikia kiasi cha sh. bilioni 8.2 kuinua zao la alizeti katika mkoa wa Singida sambamba na kuleta mageuzi makubwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi hapa nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano wa wadau wa zao la alizeti, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine alisema benki yake imejipanga kuhakikisha zao la alizeti linatoa mchango stahiki ikiwemo uzalishaji wa mafuta kula kwa wingi.

“Kama benki tumejipanga kuhakikisha zao la alizeti linatoa mchango mkubwa na hivyo tumeshatoa cha sh. bilioni 2.2 kufanikisha ununuzi wa zao hilo hapa Singida,” alisema Justine.

Mapema akiwasilisha taarifa fupi ya maendeleo ya benki na juhudi zinazofanywa na benki hiyo mkoani hapa mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Justine alisema benki hiyo imejipanga kuwa wakulima wa zao la alizeti wananufaika na zao hilo ikiwemo kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima na kuinua pato la taifa.

“Kwa kushirikiana na benki washirika tunahaidi kuwezesha ununuzi wa zao hili la alizeti ili wakulima waweze kunufaika na viwanda viweze kuzalisha mafuta kwa wingi hapa nchini,” alisema Justine.

Mtaalamu wa program za Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa hapa nchini (UNDP), Amon Manyama akizungumza katika kikao cha kuangalia vyazo vya fedha kuchangia sekta ya kilimo Jijini Arusha mwishoni mwa wiki. Katikati Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), Japhet Justine na kulia Afisa Mtendaji Mkuu na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya YYTZ Agro-processing.

Alisema moja ya kiwanda kilichojengwa kwa uwezeshwaji uliofanywa na benki hiyo kinatarajia kuzalisha tani 20 za alizeti kwa siku jambo ambalo amelitaja kuwa litawezesha ununuzi wa zao hilo kwa wingi kwa wakulima.

“Hapa kuna kiwanda tulikiwezesha kujengwa kwake na kitazalisha tani 20 kwa siku, sasa hii ni fursa kwa wakulima na niwasihi muitumie ili muweze kunufaika na uwepo wa kiwanda hiki mahali hapa,”alisema.

Aliongeza kuwa Benki hiyo pia inawezesha ununuzi wa dhana za kilimo katika maeneo mbalimbali ili kuchagiza na kuongeza ufanisi na kukifanya kilimo kiwe na tija zaidi.

“Sisi kama benki tunawezesha ununuzi wa dhana za kilimo, kwa mfano katika Wilaya ya Simanjiro tumewezesha ununuaji wa mkopo wa Matrekta 19 ambayo yatatumiwa na wakulima kwenye shughuli zao za kilimo’.

Alisema katika kuhakikisha kanda ya kati inanufaika kwa kiasi kikubwa na Benki hiyo, aliwaomba wakuu wa Wilaya wa maeneo hayo kuwapa miradi mitatu ambayo ni mifugo, kilimo na uvuvi.

“Mimi nilishafika na kukutana na wakuu wa wilaya za Kiteto na Manyara na kwenye kikao niliwaomba Wakuu wa Wilaya katika kila wilaya watupatie miradi mitatu mitatu ambayo iwe kwenye upande wa mifugo, mazao na uvuvi,” alisema Bw.Justine.

Aidha, Justine alisema zipo changamoto kubwa wanayokumbana nayo ikiwepo ucheleweshwaji wa urejeshaji wa mikopo kwa wakati jambo ambalo kwa kiasi fulani linarudisha nyuma jitahada zao.

Waziri wa Kilimo Prof Adolf Mkenda akieleza jambo mara baada ya kuongea kwenye mdahalo wa uwekezaji wa ulaya katika sekta ya kilimo uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Arusha

“Kumekuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa kurejesha mikopo kwenye vyama vya ushirika (AMCOS), kwa mfano Manyara kuna Amcos za mahindi zaidi ya miaka ambazo tunazidai takribani million 500 huku bado wakisuasua kuzilipa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Justine aliwashauri wakulima pamoja na vyama vya ushirika kuzingatia nidhamu ya fedha wanazokopeshwa kama moja ya misingi muhimu katika matumizi ya fedha za mikopo pindi wanapokabidhiwa ili kuendesha shughuli zao.