January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya KCB yazindua kiwanda cha mafuta ya kupikia Shinyanga

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Benki ya KCB imezindua rasmi kiwanda cha mafuta ya kupikia (Alizeti) kiitwacho Gilitu Enterprises LTD ambapo wamekiunga mkono kwa kukipatia pesa za kununulia mitambo na vifaa kwaajili ya uzalishaji ikiwa hadi sasa uzalishaji umeanza na mafuta yanauzwa kote Kanda ya Ziwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho kilichopo Mkoani Shinyanga, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Cosmas Kimario amesema mikopo yao inalenga sehemu tofauti tofauti ikiwemo sekta ya biashara ambapo ilikwenda sambamba na serikali ya awamu ya tano juu ya uchumi wa viwanda nchini na sasa wanaenda sambamba na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais samia ya kusema kazi iendelee;

“Mikopo yetu imelenga sekta tofauti tofauti kwa mfano mkopo huu umelenga sekta ya wafanyabishara wa viwanda na ilikwenda sambamba na serikali ya awamu ya tano wakati ule ikiwa ni uchumi wa viwanda na awamu hii ya 6 ambayo inaongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu hassan ikisema kazi indelee”

Aidha mbali na kiwanda walichokizindua mkoani hapo wameendelea kuviunga mkono viwanda mbalimbali mkoani Dar es Salaam kwa kuwapa mikopo iliyo nafuu itakayowasaidia kuzalisha viwanda vingi na kuongeza uzalishaji nchini;

“Mbali na kiwanda hicho, vipo viwanda vingine ambavyo tumekuwa tukivisaidia ambavyo vipo Dar es salaam ambapo tunazungumza na wateja ili kuwapa mikopo ambayo ni nafuu itakayoweza kuwasaidia kutengezeza viwanda, kuzalisha ndani na kuwaondolea serikali mzigo wa kutumia fedha za kigeni kuagiza vitu kutoka nje”

Aidha amewakaribisha wafanyabiashara wote waliopo viwandani, katika sekta ya usafiri, ujenzi, hospitali, n.k kuja kuwekeza ili kuongeza viwanda na kuchochea pato la Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kupikia kutoka Shinyanga, Giritu Nhila Makula alisema kufuatia viwanda vya mafuta kuzidi kuongezeka nchini hasa kupitia kiwanda hicho cha Gilitu, kutasaidia sana kupunguza uhaba wa mafuta nchini Tanzania;

“Japokuwa tunaambiwa watanzania viwanda vyetu vinasambaza mafuta kwa asilimia 40 lakini kwa sasa naona viwanda vinazidi kuwa vingi hivyo serikali wafanye tathimi upya, kwa sasa tunasambaza mafuta kila sehemu hivyo kwangu mimi ninavyoona uhaba wa mafuta haupo tena”alisema Mkurugenzi huyo na kuongeza

“Mafuta yetu bei yake ipo chini tofauti na nje, ambapo kwenye Lita 20 bei yetu ni tofauti karibu 15,000”

Alisema watanzania tunatabia ya kutojiamini kama tunaweza ambapo watu wameshajikaririrsha kwamba mali zinazotoka nje ndiyo zenye ubora kuliko zinazozalishwa ndani lakini ukweli ni kwamba mafuta ni mengi nchini na yanazalizwa kwa ubora.

Mkurugenzi huyo amewawataka watanzania kununua mafuta ya ndani kwasababu yana ubora unaostahili.

Naye Meneja Benki ya KCB tawi la Mwanza, Emmanuel Mzava amesema wao kama KCB wamekuwa na uzoefu mkubwa wa kuielewa biashara ya mteja, kumpa bidhaa sahihi na kupata masoko.

“Katika wateja ambao tumekuwa nao na mmoja kati ya mteja ambaye leo tunafanya uzinduzi wa hiki kiwanda tunaweza tukaelezea kuwa tunauzoefu mkubwa sana wa kuielewa biashara ya mteja, kumpa njia za kutatua na kumpa bidhaa sahihi kwasababu mtu anapofanya uwekezaji wa kiwanda ni tofauti na mtu anaefanya biashara ya duka ya kuuza bidhaa na kupokea, uwekezaji wa kiwanda ni wa mda mrefu kwahiyo lazima ukae na uelewe mteja anahitaji nini vilevile umsaidie mteja apate bidhaa sahihi na mteja kutafuta masoko na aweze kujua biashara anaipeleka wapi”

Aidha amesema wao kama KCB wateja ni wabia kwa maana ya kwamba wanashirikiana nao katika kila kitu, wanaielewa biashara ya mteja kwamba inahitaji nini ambapo wao wanakua watatuzi kwa mteja kwa maana ya kwamba mteja anapopata changamoto wao ndiyo wanatoa njia ya kutatua changamoto hiyo.

Naye Mkuu wa Kitengo cha biashara za kati na ndogondogo wa Benki ya KCB, Abdul Juma ametoa wito kwa wafanyabiashara wote wakubwa, wa kati na wadogo kuja kuwekeza na KCB kwasababu nafasi ipo siyo tu kwa wafanyabiashara wa kanda ya ziwa bali Tanzania nzima, kwasababu KCB ni Benki kubwa inayopatikana kila sehemu hivyo wanafungua Milango na fursa kwa wafanyabiashara kuja na mawazo ambayo yatasaidia kuokoa fedha.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara Shinyanga, Dkt. Kulwa Meshack amesema katika kipindi cha COVID-19 na
vita ya Ukraine pamoja na Urus biashara ya mafuta imekuwa na changamoto kubwa kwasababu mafuta mengi yaliyokuwa yanakuja kutoka nje ya nchi sasa yamekuwa hayafiki na kwasababu hiyo mafuta pekee ambayo ni kimbilio ni mafuta ambayo yanazalishwa hapa nchini ikiwemo mafuta hayo ya alizeti ambayo hayana madhara mwilini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Cosmas Kimario (kushoto), akiwa na Mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha mafuta ya kupikia kutoka shinnyanga, Giritu Nhila Makula (kulia) wakizindua kiwanda hicho cha kuzalisha mafuta ya kupikia kiitwacho Gilitu Enterprises LTD ambapo Katika uzinduzi huo wameambatana na Mwenyekiti wa wafanyabiashara Shinyanga, Dkt. Kulwa Meshack (Aliyevaa barakoa) na Mkuu wa kitengo cha biashara za kati na ndogondogo wa Benki ya KCB, Abdul Juma (wa kwanza kushoto)
Kiwanda cha mafuta ya kupikia kiitwacho Gilitu Enterprises LTD kilichozinduliwa Mkoani Shinyanga