November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya KCB yazindua huduma za Bima

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Wito umetolewa kwa wafanyakazi na wadau wote wa bima kuunga mkono jitihada za dhati zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na Benki ya KCB ili kuongeza uelewa na upatikanaji rahisi wa bima kwa Watanzania kwani umuhimu wa bima ni mkubwa

Wito huo umetolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Juma Abdul wakati wa uzinduzi wa huduma za bima za Benki ya KCB (bancaassurance)

Juma alisema wao Kama Benki ya KCB wanashauku kubwa Sana ya utoaji huduma za Bima kwasababu wanaamini kwamba huduma za bima Zina mchango mkubwa katika maisha ya Watanzania na zinachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la Pato la Taifa

Aidha Mwakilishi huyo alisema watahakikisha huduma hiyo ya bima inawafikia walengwa kwa wakati na muda hitajika;

“Sisi KCB Bank ni jukumu letu kuhakikisha huduma hii inawafikia walengwa kwa wakati na kiwango hitajika ili kuunga mkono serikali na kubariki jitihada zote zinazochukuliwa kukuza uchumi wa nchi yetu”

Aidha alisema Bima ni muhimu sana katika kulinda thamani zetu, majanga Kama ajali za barabarani, moto, vifo na mengineyo yanaweza kupatiwa suluhisho na kinga ya uhakika pale yatakapotokea;

“Ajali na majanga havina taarifa kwamba ni muda gani au siku gani vitakuja na haviwezi kutabirika kwamba vitakukuta ukiwa na hali gani, hivyo ni muhimu kujipanga mapema na namna ya kuvikabili kabla havijatokea”

Juma alisema Benki ya KCB Tanzania imepewa rasmi mamalaka na serikali kupitia mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania kutoa huduma mbalimbali za bima kutoka Benki Moja kwa Moja kwenda kwa mteja hivyo watahakikisha wameongeza wigo wa upatikanaji wa huduma za bima kwa Watanzania

Kwa upande wake Meneja wa kitengo Cha bima kutoka KCB Bank, Pamela Urio amesema uzinduzi huo ni hatua muhimu kwani utawawezesha watanzania kupata Huduma za bima katika matawi yote ya KCB

Naye Afisa Mtendaji Mkuu kutoka Jubilee insurance, Helena Mzena ameipongeza Benki ya KCB kwa kuja na Bima hiyo kwasababu inaenda kusaidia kuendelea kuhudumia wateja wao lakini pia wateja hao kuweza kubaki na KCB bila kuhamahama

Aidha Helena aliwahasa wananchi kukata bima hasa bima ya maisha kwani ni muhimu na ni salama.

Ikumbukwe kuwa TIRA, chini ya serikali awamu ya sita kupitia wizara ya fedha na mipango imeweka mikakati madhubuti ya kuongeza uchangiaji wa sekta ya bima katika uchumi wa Taifa, kwani mpaka sasa sekta ya bima hapa nchini inachangia takriban 0.57% ya uchumi wa Taifa letu