April 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Benki ya CRDB kufungua tawi Congo ya DRC

Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Arusha

MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela amesema Oktoba, mwaka huu wanaanza kutoa huduma za kibenki nchi ya Congo ya DRC ili kuongeza wigo wa utoaji huduma kwa nchi za Afrika Mashariki, huku Congo DRC akiwa ni mwanachama mpya kwenye jumuiya hiyo.

Kabla ya Congo DRC, tayari walikuwa nchi ya Burundi kwa miaka 10 sasa, huku CRDB ikiwa ni benki ya tatu katika kutoa huduma bora nchini humo, huku dhamira yake ni kuwa wa kwanza nchini humo katika kutoa huduma

Hayo yalisemwa leo Mei 18, 2022 kwenye mkutano wa Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB na waandishi wa habari uliofanyika jijini Arusha, ambapo mkutano huo, pamoja na mambo mengine, ni kuwatambulisha wanahisa wa benki hiyo kuwa Mei 21, mwaka huu kutafanyika Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB, ambapo kabla ya mkutano huo, utatanguliwa na semina kwa wanahisa Mei 20, mwaka huu, ambapo mgeni rasmi kwenye semina hiyo atakuwa Spika wa Bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson.

“Benki ya CRDB tunatarajia kufungua tawi katika nchi ya Burundi. Na sisi katika nchi ya Burundi ni wa tatu katika utoaji huduma bora za kibenki, na nia yetu ni kuwa namba moja katika utoaji huduma hiyo” alisema Nsekela.

Nsekela alisema wanampongeza Rais wa Awamu ya Sita Samia Suluhu Hassan katika kujipambanua kuhusu Sekta Binafsi, kwani katika uongozi wake, ametoa kipaumbele kwa Sekta Binafsi na kuifanya sekta hiyo kuonesha mafanikio ndani ya muda mfupi ikiwemo kuifanya sekta hiyo kukua na kuzalisha faida ikiwemo Benki ya CRDB.

“Rais ameonesha kuijali na kuipa kipaumbele Sekta Binafsi. Amefanya shughuli za kiuchumi kusisimka kwa shughuli za ndani ya nchi na nje ya nchi. Sisi kama Sekta Binafsi, jambo hili tulipongeza, na limeweza kutupa nguvu ya kufanya vizuri katika shughuli zetu za kila siku” alisema Nsekela.

Nsekela alisema Benki ya CRDB imeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa watu 3,600, lakini wametoa kazi kwa wakala 22,000, na kama wameweka watu wawili wawili, basi itakuwa ni watu 44,000 wamepata ajira.

“Lakini katika mikopo tunayotoa, tumewezesha kutoa mikopo hiyo kwa wamachinga na wajasiriamali wengine. Nia yetu ni kuiwezesha jamii na kuinuka kiuchumi” alisema Nsekela, na kuongeza kuwa katika kuonesha kila wanachokifanya ni kwa ajili ya wananchi, kauli mbiu ya Mkutano Mkuu mwaka huu ni ‘Thamani Endelevu’.

Alisema ukuaji endelevu unaonekana katika matokeo ya kifedha, na unaakisiwa katika ukuaji wa uwiano wa faida kabla ya kodi na wastani wa fedha za wanahisa (ROE), ambapo mwaka 2021 ilikuwa asilimia 22 kulinganisha na asilimia 16.3 ya mwaka 2022.

Nsekela alisema thamani ya hisa sokoni, ambapo hivi karibuni baada ya kutangaza matokeo ya fedha yaliyokaguliwa, imepanda hadi sh. 380 kutoka sh. 140.

“Lakini pia tumekuwa tukishuhudia ukuaji endelevu katika gawio kwa wanahisa, ambapo mwaka huu tumeona bodi imekuja na pendekezo la sh. 36, ikiwa ni ongezeko la asilimia 64 kulinganisha na sh. 22 iliyotolewa mwaka 2021” alisema Nsekela.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (katikati), akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha. Pamoja na mambo mengine, amezungumzia Mkutano Mkuu wa 27 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB utakaofabyika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Ukumbi wa Simba Mei 21, 2022, huku akiwataka wanahisa kuhudhuria mkutano huo. Na wale watakaoshindwa kufika, watafuatilia kwenye mtandao (Hybrid Meeting). Wengine ni Mwenyekiti Benki ya CRDB Dkt. Ally Laay (kushoto), na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CRDB Tully Mwambapa (kulia). (Picha na Yusuph Mussa).
Baadhi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (hayupo pichani), alipokuwa anazungumza leo Mei 18, 2022 jijini Arusha juu ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa utakaofanyika Mei 21, 2022. (Picha na Yusuph Mussa).
Baadhi ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa Benki ya CRDB wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela (hayupo pichani), alipokuwa anazungumza leo Mei 18, 2022 jijini Arusha juu ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa utakaofanyika Mei 21, 2022. (Picha na Yusuph Mussa).