May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bei ya Mafuta yazidi kushuka

Na Penina Malundo, timesmajira

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetangaza bei mpya za ukomo wa mafuta ya Diseli na Petrol na Mafuta ya Taa hapa nchini zitakazo anza kutumika kuanzia  leo (jumatano).

Taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Mamlaka hiyo imesema bei ya mafuta ya rejareja ya dizeli kwa Dar es Salaam na Tanga kwa Novemba 2022 imepungua kwa shilingi 31/lita na 34/lita, sawia ikilinganishwa na bei hizo kwa Oktoba 2022 kwa sababu ya ruzuku.

Imesema  bei ya rejareja ya mafuta ya petroli kwa Bandari ya Dar es Salaam ingeongezeka kwa shilingi 110 kwa lita, hatahivyo, Serikali imetoa ruzuku ili bei iliyopo ya Oktoba 2022 isibadilike. 

“Kwa upande wa Mtwara, hakuna meli ambayo imehusishwa kwenye bei kwa Novemba 2022 kwa sababu meli inategemewa kushusha mafuta mwishoni mwa Novemba 2022 na mafuta yake yatatumika Desemba 2022,”Imesema na kuongeza

“Mabadiliko ya bei kwa Novemba 2022 kwa Mtwara ni kwa ajili ya kuhusisha taarifa sahihi ya meli husika iliyotumika kwenye bei za Oktoba 2022,”imesema

Imesema bei ya mafuta ya taa na bei ya petroli kwa Tanga imepungua kwa shilingi 164kwa lita na shilingi 118 kwa lita ukilinganisha na bei zilizopita kwa sababu ya wastani wa bei ndogo zaidi ya mafuta yaliyosafishwa katika soko la dunia na gharama za usafirisha kwa bandari ya Tanga. 

Imesema katika kutekeleza bei hizi, wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kwa jumla na rejareja pamoja na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuzingatia  kuwa  bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko. 

“EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. Taarifa hizi zina lengo la kuwasaidia wadau kufanya maamuzi stahiki kuhusu manunuzi ya bidhaa za mafuta,”imesema na kuongeza

“Kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo (Price cap) au kushuka chini ya bei iliyoruhusiwa (Floor Price) kama ilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za EWURA za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022 zilizotangazwa kupitia Magazeti ya Serikali Na. 2A na 57 Januari 3,2022 na Januari 28, 2022, sawia,”imesisitiza

Aidha imesema  Vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana na yakionesha bei ya mafuta, punguzo, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika. Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. “Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,”imesema