Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online Tanga
Mamlaka ya bandari Tanzania TPA, Mkoa wa Tanga imesema bandari hiyo itaanza kupokea meli kubwa za magari ifikapo mwezi Mei mwaka huu baada ya gati mbili za kisasa kukamilika jambo ambalo limeilazimu bandari hiyo ya Tanga kufikiria kulitumia eneo la Mwambani kwenye shughuli za bandari ili kuepusha msongamano mkubwa unaoweza kutokea kwenye eneo la bandari linalotumika hivi sasa.
Meneja wa bandari ya Tanga Masoud Mrisha ameyasema hayo wakati alipokuwa bandarini hapo na wadau wa bandari hiyo ambapo amesema eneo hilo la Mwambani ni sehemu ya bandari ya Tanga na lina ukubwa wa hekta 176 hivyo kufuatia mpango huo wanataka kulitumia eneo hilo la mwambani kufanyia shughuli zao ikiwemo upakiaji wa mizigo kwenye makontena.
Meneja Mrisha amesema kuwa eneo hilo la Mwambani litaweza kusaidia kwa kiwango kikubwa kuepusha msongamano unaoweza kujitokeza katika bandari ya hivi sasa.
“Tunatarajia ifikapo mwezi Mei kuanza kuhudumia meli za magari na tumependelea vilevile hayo magari tutaweza kuyapeleka na, kuyahifadhi katika eneo la Mwambani na leo hii tuliwakaribisha wadau kuwasikiliza hoja zao kuhusiana na utumiaji au maboresho ya bandari hii ya Tanga ambapo tumewaeleza jinsi mradi ulivyo mpaka sasa awamu zote 3,”amesisitiza Meneja Mrisha.
Meneja Masoud alisema kwamba wamesikiliza na, kuzipokea hoja za wadau hao huku akiahidi kuzifanyia kazi ili waweze kuitumia bandari ya Tanga ili iweze kutoka kwenye shehena wanayoihudumia hivi sasa kutoka tani laki 7 na hamsini hadi kufikia tani milioni 3.
Kaimu Mkurugenzi wa masoko na uhusiano kutoka mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania Nikodemas Mushi amesema kufuatia maboresho hayo wanatarajia kwenda nchi za Rwanda, Burundi, Zambia na Congo DRC ili kuweza kuhamasisha kupata wateja wapya lakini vilevile kuwarejesha wateja ambao walikuwa wakitumia bandari hizo hapo awali ambao walioacha kutokana na changamoto mbalimbali.
Alisema kupitia kikao hicho lengo lao lilikuwa ni kuondoa nafasi ya maswali hoja na changamoto mbalimbali ambazo hazijaweza kutoka upande mmoja kwenda mwingine ambapo wadau hao wameweza kutoa maoni, ushauri, wameuliza maswali na kupatiwa majibu.
“Huu ni moja ya mkakati wa kimasoko kukutana na wateja kuzungumza nao kutengeneza mkakati wa pamoja wa utekelezaji ni moja ya mbinu za kuongeza masoko kwani serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika mamlaka ya bandari Tanzania nikimaanisha bandari zote za TPA ikiwemo bandari ya Daresalaam, Tanga, Kigoma, Mtwara na Ziwavictoria kule Mwanza zote zimefanyiwa upanuzi mkubwa na mazoezi yanaendelea katika hatua mbalimbali, “amesisitiza Mushi.
Awali wakizungumzia maendeleo ya bandari hiyo wadau hao akiwemo Athuman Semainda na Liliani Mbwambo walisema hatua iliyofikiwa hivi sasa ya bandari ni ushahidi tosha ya kwamba uchumi wa Tanga na Taifa kwa ujumla unakwenda kuongezeka.
Liliani Mbwambo amesema kuwa wanashukuru hivi sasa wameshaona muonekano kwa uhalisia na matumaini na mategemeo yao kutokana na jinsi walivyoambiwa bandarini hapo ni kwamba huko wanapokwenda biashara inakwenda kuongezeka.
Serikali imewekeza fedha nyingi katika maboresho ya upanuzi wa bandari ya Tanga kwa lengo la kutaka kuona ni kwa kiwango gani bandari hiyo inaweza kuhudumia meli kubwa na hivyo kuongeza pato Taifa.
More Stories
Wassira:Waliopora ardhi za vijiji warudishe kwa wananchi
Rais Samia apongezwa kwa miongozo madhubuti ya ukusanyaji wa kodi
Mwenda:Siku ya shukrani kwa mlipakodi ni maalum kwaajili ya kuwatambua,kuwashukuru