December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Balozi wa Marekani apongeza uendeshaji michakato ya kisiasa nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Balozi wa Marekani nchini Mhe. Dkt. Donald Wright amepongeza uendeshaji wa michakato ya kisiasa inavyoendeshwa nchini Tanzania.

Balozi Wright ameyasema hayo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Wright amesema anaridhishwa na jinsi hali ya kisiasa ilivyo hapa nchini na kuongeza kuwa anaunga mkono michakato ya kisiasa inavyoendeshwa nchini na kuelezea kuridhishwa kwake na hali hiyo.

Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani kwa maslahi ya pande zote mbili.

Naye Waziri Mulamula amemuahidi Dkt. Wright kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake wakati wote hapa nchini.

Katika tukio jingine, Waziri Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Mhe. Elisabeth Jacobsen na kujadili masuala ya ushirikiano katika masuala ya amani na usalama, jinsia na uwezeshaji wa wanawake.

Pia, Waziri Mulamula amekutana kwa mazungumzo na Afisa kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) Bibi. Jacqueline Machangu-Motcho na kujadili masuala ya ushirikiano baina ya mfuko huo na Tanzania.