Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
Waziri wa Fedha,Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ameonesha kuridhika na usimamizi wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) katika matumizi ya Moduli ya kupokea na kushughulukia malalamiko na rufaa katika mfumo wa NeST.
Balozi Omar ametoa pongezi hizo alipotembelea Banda la Maonesho la PPAA lililopo ndani ya Banda la Wizara ya Fedha julai 02, 2026 kwenye Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es Salaam ambapo PPAA inaendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusu huduma na majukumu yake.
“Hongereni kwa kazi nzuri ya kutoa elimu kwa Umma, nimejulishwa kuwa Kwa sasa baada ya matumizi ya Moduli kuanza hakuna longolongo kwenye mashauri yatokanayo na michakato ya ununuzi wa umma, endeleeni kusimia vyema matumizi ya Moduli vyema,” amesema Balozi Omar

Kwa Upande wake Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Sheria PPAA,Agnes Sayi ambaye alikuwa anamwakilisha Katibu Mtendaji wa PPAA, Bw. James Sando alimweleza Mhe. Waziri kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/26 Mamlaka ya Rufani imepokea malalamiko takribani 158 yaliyowasilishwa kupitia Moduli hiyo na kuyashughulika kwa wakati kama Sheria ya Ununuzi wa Umma inavyoelekeza.
“Waziri matumizi ya moduli yanasaidia Taasisi za Serikali na wazabuni/wadau wa ununuzi kwa ujumla kuokoa muda, gharama, inaongeza uwazi na uwajibikaji, inawezesha utunzaji wa kumbukumbu na kuiwezesha PPAA kutoa hukumu kwa haki na wakati,” amesema Sayi

Pamoja na mambo mengine,Balozi Hamis ameielekeza PPAA kuendelea kutoa elimu zaidi kwa Umma kuhusu majukumu yake pamoja na matumizi ya Moduli ili kutoa fursa zaidi kwa wazabuni na wadau wa ununuzi wa umma kuendelea kudai haki zao pale ambapo hawakuridhishwa na michakato ya ununuzi wa umma.
Kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026 Mamlaka ya Rufani imefanikiwa kutoa elimu kwa wazabuni 1,907 pamoja na watumishi 705 wa idara za ununuzi na sheria katika maeneo mbalimbali nchini katika kanda za Kaskazini, Ziwa, Nyanda za Juu Kusini, Kati, na Pwani pamoja na mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa na Mwanza.


More Stories
Wizara yahamasisha Watoto kuhusu Nishati Safi
ETDCO yaonesha Mafanikio yake Sabasaba
Masaju apongeza kazi ya OSHA