December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Bagamoyo Sugar yaanza ujenzi wa uwanja

Na Omary Mngindo, TimesMajira Online, Bagamoyo

KAMPUNI ya Bagamoyo Sugar inayojihusisha na kilimo cha Miwa kwa ajili ya kutengeneza Sukari katika eneo la Razaba Maakurunge, wameanza ujenzi wa uwanja wao wa michezo.

Ujenzi wa uwanja huo unatajwa na kuthibitisha ni namna gani uongozi wa Kampuni ya Bakhresa Group chini ya Mkurugenzi Mkuu Said Salim Bakhresa unavyothamini michezo kwa watumishi wanaofanyakazi kwenye Makampuni hayo.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mahusiano Makampuni hayo Hussein Sufiani Ally, alipokuwa akitoa taarifa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo alipotembelea ujenzi wa majengo ya kampuni hiyo.

Amesema, wakati ujenzi wa majengo ya Kampuni hiyo inayozalisha Miwa kwa ajili ya sukari ukiendelea, tayari maandalizi ya ujenzi wa uwanja ndani ya mashamba hayo ya miwa na watahakikisha unaendelea kwenda sambamba lengo likiwa ni kuwapatia fursa wafanyakazi wao kushiriki michezo.

“Kama unavyojionea katika hii ramani ya ujenzi wa majengo mbalimbali katika Kampuni yetu, pia suala la michezo tumelipatia nafasi yake, katika hii ramani hapa ndipo utakapojengwa uwanja, tulipokuwa tunatoka ofisini uwanja upo mkono wa kushoto umeshajazwa kifusi na magoli tayari,” amesema Sufiani.

Kwa upande wake Mhandisi Ndikilo ameupongeza uongozi wa Kampuni hiyo chini ya Mkurugenzi wake Bakhresa na viongozi mbalimbali kwanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho chenye majengo makubwa na ya kisaasa, sanjali na kujali afya za wafanyakazi kwa kujenga uwanja wa michezo.

“Utanifikishia salamu zangu kwa Mkurugenzi Mkuu Said Salim Bakhresa kwa ujenzi wa kiwanda kikubwa hapa Bagamoyo, amekwenda mbali zaidi ya wazo kuanza maandalizi yaa ujenzi wa uwanja kama inavyoonesha kwenye ramani yenu hivyo hongereni sana lakini pia napenda kuyataka makampuni mengine kuiga mambo haya mema na mazuri mnayoyafanya,” amesema Mhandisi Ndikilo.