Na Joyce Kasiki,Timesmajjira online,Dodoma
SERIKALI imesema,Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Nchini (EWURA) imetoa leseni nne za kutoa huduma ya majisafi na usafi wa Mazingira lakini pia imetathimini na kuidhinisha bei mpya za huduma ya maji kwa  Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira saba katika mwaka 2023/2024.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2024/2025.
Amezitaja leseni nne za kutoa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kuwa ni katika Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira za Miji ya Rombo, Kyela- Kasumulu, Njombe na Busega.
Aidha, alisema Mamlaka za Maji zilizofanyiwa tathimini na kuidhinishiwa bei mpya za huduma ya na EWURA ni Dodoma, Makonde, Sumbawanga, Orkesumet, Mombo, Bariadi na Lindi.
Vilevile alisema,katika kipindi hicho, EWURA ilifanya mapitio ya mipango- biashara ya mamlaka za majisafi na usafi wa mazingira 11 na kuidhinisha mikataba sita ya huduma kwa mteja kwa mamlaka za Musoma, Liwale, Makambako, Lindi, Biharamulo na Geita.
 Waziri Aweso amesema  katika mwaka 2022/23,  EWURA ilitoa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira ambayo inaainisha utendaji wa mamlaka za maji nchini na kuweza kusaidia
Wizara pamoja na wadau wa sekta ya maji katika kuandaa na kutekeleza mipango mbalimbali ya kuimarisha na kuboresha huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
“Taarifa hiyo, imebainisha kuwepo kwa mafanikio katika ongezeko la uzalishaji wa maji kwa lita bilioni 7 sawa na asilimia 1.78, kuongezeka kwa uwezo wa miundombinu ya kuzalisha maji kwa lita bilioni 126 sawa na asilimia 16.94 na kuongezeka kwa idadi ya wateja wanaopata huduma ya maji kwaasilimia 11.
Aidha, taarifa imebainisha changamoto zinazokabili mamlaka za maji ambazo ni pamoja na kuongezeka kwa upotevu wa maji ambao umefikia asilimia 37, upungufu wa miundombinu ya huduma ya usafi wa mazingira; na uwiano usioridhisha wa ongezeko la mahitaji ya maji ikilinganishwa na uzalishaji wa maji.
More Stories
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo