November 7, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Askofu: Watanzania tumlilie Mungu

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online-Tanga

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Kaskazini mwa Tanzania wa Kanisa la Waadventista Wasabato, Dkt. Godwin Lekundayo amesema,licha ya jitihada zinazofanyika za kupambana na ugonjwa wa Corona bado Watanzania wanayo nafasi ya kuendelea kufanya maombi ili kukabiliana na ugonjwa huo kwa awamu ya tatu.

Tayari Tanzania imeshabainisha kuwa na wagonjwa kadhaa wa Corona ambao wengine wapo kwenye mashine za kupumulia na wengine wakiendelea na matibabu.

Askofu huyo ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akihutubia mamia ya waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato walipokuwa kwenye sherehe za vibanda maarufu kama makambi yaliyoshirikisha mitaa mbalimbali ya jiji la Tanga.

Askofu huyo amesema kwamba, ipo sababu ya msingi ya watanzania kufanya maombi huku wakiendelea kujikita katika unawaji wa mikono na sabuni kwa kutumia maji tiririka pamoja na uvaaji wa barakoa.

“Ugonjwa wa Corona upo na kila mtanzania anapaswa kuona namna gani ya kupambana nao ikiwa ni pamoja na kunawa mikono na sabuni, kukaa umbali unaokubalika kiafya, lakini pia na kuvaa barakoa bila kusahau maombi,”amesisitiza Askofu huyo.

Dkt.Lekundayo aliwataka waumini wa kanisa hilo na wananchi kuendelea kuchukua tahadhiri ya ugonjwa huo.

“Tunawaomba waumini wetu kuchukua Tahadhiri zote ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na Sabuni na kujiepusha na misongamano,”alisisitiza.

Kuhusu siku 100 za Rais madarakani Askofu huyo amesema tangu Rais Samia ameanza kufanya kazi ameshajipambanua kwenye masuala mbalimbali ikiwemo suala la uhuru wa kujieleza.

Amesema, licha ya kwamba ameonekana kuendeleza miradi ya mtangulizi wake, lakini pia ameonyesha kuwa mbunifu kwenye vitu vyake mwenyewe lengo likiwa ni kuwapeleka watanzania mahali wanapohitaji kiuchumi sambamba na kuimarisha uchumi wa nchi.

Akizungumzia uongozi huo wa Rais Samia Suluhu Hassan,Askofu Lukendayo amesema, Rais huyo ameonyesha mwelekeo mpya wa Taifa na kwamba kanisa hilo litaendelea kumuombea kiongozi huyo na Serikali yake ili Mungu aendelee kumuongoza.

“Tumeona ameendelea kutupa uhuru wa kuabudu kama alivyofanya mtangulizi wake hivyo sisi tutaendelea kushirikiana nae,”amesema.

Askofu huyo ameitaka jamii hususani vijana kubadilika na kuacha kujihusisha na mambo yanayoharibu mfumo wa maadili ikiwemo matumizi ya vilevi mbalimbali hususani dawa za kulevya, matumizi mabaya ya lugha pamoja na mitindo mibaya ya mavazi.

Dk.Lekundayo amesema, mfumo wa utandawazi umeendelea kuitesa jamii kubwa ya Watanzania hivyo wao kama kanisa wameliona hilo na kuanza kuchukua hatua ya kukemea vikali.

Kwa upande wake Mchungaji Musa Nzumbi ambaye ni Askofu wa jimbo dogo la Kaskazini Mashariki mwa Tanzania wa Kanisa la Waadventista Wasabato amesema, katika ibada hiyo pamoja na mambo ya kiimani, lakini pia wameshiriki katika uchangiaji wa damu pamoja na kula chakula cha mchana na watoto yatima.

Sherehe za vibanda maarufu kama Makambi huadhimishwa kila mwaka na Jumuiya ya Waadventista Wasabato lengo likiwa ni kuwasogeza karibu na Mungu na kuwafundisha mafundisho mbalimbali yanayolenga kuwaimarisha kiafya na kiroho ambapo Katika sherehe hizo zilizoanza Juni 26 na zinatarajiwa kumalizika Julai 3, mwaka huu katika Jiji la Tanga.