June 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

IGP atoa siku 7 kukamatwa watoto wa ibilisi

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online

MKUU wa Jeshi la Polisi Nchini Tanzania, IGP Simon Sirro ametoa siku saba kwa Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga, Blasius Chatanda kuhakikisha vikundi vya uhalifu vinavyojiita watoto wa ibilisi vinamalizika haraka katika jiji la Tanga.

Kamanda Sirro ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao kilichoshirikisha Wenyeviti wa serikali za mitaa, watendaji wa kata na madiwani wa Halmashauri ya jiji la Tanga ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kutembelea na kukagua hali ya ulinzi katika mikoa mbalimbali nchini.

IGP Sirro ametoa agizo hilo kufuatia kuibuka kwa kundi la vijana wadogo wanaotembea kati ya 20 na kuendelea ambao hujihusisha na kufanya vitendo vya kihalifu huku wengine wakiwajeruhi baadhi ya watu katika maeneo mbalimbali.

Kamanda Sirro amesema, Jeshi la Polisi limeweza kupambana na matukio makubwa katika Mkoa wa Tanga hivyo kikundi hicho kinachojiita watoto wa ibilisi hakitoweza kufanya vitendo vyovyote vya kihalifu kuanzia sasa kwani jeshi hilo limejipanga kuwawajibisha.

“Kuhusu vikundi vya watoto wa Ibilisi maelekezo yangu kwa RPC nawapa wiki moja hiyo habari ya watoto wa ibilisi sitaki kusikia na kama watakuwepo katika huu mji nina uwezo wa kuingia ndani ya siku mbili tukamaliza, “alisistiza IGP Sirro.

Aliongeza kuwa, hatuwezi kukaa na watoto wetu tena wadogo kisha tuwaite watoto wa ibilisi, viongozi wenzangu ipo haja ya kutazama malezi yetu lakini pia kwanini basi mnazaa watoto ambao hamuwezi kuwapa mahitaji yao kisha wanarudi kuwasumbua watanzania wenzao hamuwezi kuwasomesha, kuwalisha na kuwatunza matokeo yake wanajiingiza kwenye uhalifu hii siyo sawa jaman wazazi wenzangu, “amesema Kamanda Sirro.

Kamanda Sirro aliwataka wazazi na walezi mkoani Tanga kuhakikisha watoto wao wasiwe kero kwa wengine kwani ni aibu kuona vijana wadogo wanatia dosari mji wa Tanga hivyo amesisitiza suala la kwanza kuwa ni kuzingatia elimu kwa watoto wao.

“Hii elimu ipelekeni kwenye mitaa yenu ishu siyo kuzaa wajue umuhimu wa kulea watoto wao kama tumeweza kupambana na matukio makubwa ndani ya Tanga hii hawa watoto wa ibilisi sitaki kuwasikia ndani ya wiki moja,”amesisitiza Sirro.

Mbali na kutoa onyo hilo IGP Sirro amesema, ni lazima viongozi wafanye mikutano na wananchi wao juu ya usalama uliopo na badala yake wasisubiri tu wananchi wawapelekee taarifa kwani wananchi wengine ni walemavu hawawezi kutoka kwenye maeneo yao.

“Tukienda kule kwa wananchi matatizo tutayamaliza kule kule lakini tukiwasubiria tutaendelea kuyasikia tukasikilize wananchi wetu ili tusonge mbele na tuweze kuijenga Tanzania yetu, “amebainisha IGP Sirro.

Akizungumzia makosa ya kubaka, ushoga, kulawiti Kamanda Sirro alisema makosa hayo yanatokana na maadili mabovu waliyonayo hivyo polisi hawawezi kuyamaliza peke yao hivyo viongozi wa dini, wazazi, polisi, na jamii yote kwa ujumla wanapaswa kuwa na nguvu ya pamoja ili kuyamaliza.

Aidha,Kamanda Sirro amemtaka RPC kuchagua kata 10 kati ya 27 zilizopo za mfano na kupeleka polisi kata watakwenda kusaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwa wananchi na watakapoona kuna haja ya kuongeza nguvu kwenye kata yeyote basi jeshi la polisi litafanya hivyo.

Hata hivyo Kamanda Sirro alimtaka Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Tanga Leopord Fungu kuhakikisha anashirikiana na timu yake kufanya operesheni ya kukagua pikipiki ambazo zimekuwa zikitumika kwenye vitendo vya uhalifu ambavyo vimekuwa ni kero kwa wananchi.