Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online
Ugonjwa wa saratani ya matiti ni saratani inayoanzia kwenye seli zilizoko kwenye matiti na kwa asilimia kubwa waathirika wa ugonjwa huo ni wanawake.
Daktari Bingwa wa upasuaji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, Dkt.Athanas Ngabakubi,amezungumzia ugonjwa huo,wakati wa mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya namna ya kuandika habari sahihi za afya hususani za ugonjwa wa saratani kupitia mradi Mtambuka wa Saratani Tanzania (TCCP) ambao unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) na Aga Khan Foundation (AKF).
Dkt.Ngabakubi,anaekeza kuwa kati ya watu waliopata saratani ya matiti, asilimia 1 ni wanaume na kwa mwaka 2018, saratani ya matiti ilikuwa ni asilimia 11.6 ya saratani zote zilizo wapata watu.
Ambapo saratani hiyo ya matiti ilisababisha asilimia 6.6 ya vifo vyote vya saratani duniani huku maabukizi mapya kwa mwaka 2020 ni 3992 ambayo ni asilimia 9.9 ambapo idadi ya vifo ni 1973 ambayo ni asilimia 7.3.
Dalili za ugonjwa wa saratani ya matiti
Dkt.Ngabakubi anaeleza kuwa ugonjwa ukiwa kwenye hatua za awali, mtu anaweza asiwe na dalili zozote (anaweza asiwe na maumivu kwenye titi na eneo kuzunguka titi).
Anaendelea kueleza kuwa dalili zinazoweza kujitokeza ni pamoja na uvimbe au vivimbe kwenye titi au matiti,titi kubadilika umbo, ukubwa na mwonekano.
Pia titi kuvimba, kuwasha,kubadilika kwa ngozi ya titi na kuwa na madoa au vishimo (kama ganda la chungwa),kutokwa na majimaji au damu kwenye chuchu,kuchubuka kuzunguka chuchu, chuchu kuingia ndani pamoja na chuchu kupata kidonda.
Vihatarishi vya saratani ya matiti visivyoweza kuzuilika
Dkt.Ngabakubi, anaeleza kuwa visababishi vinavyoongeza uwezekano kupata saratani ya matiti ni pamoja na jinsi ambapo wanawake wako hatarini zaidi kuliko wanaume.
Umri kuwa na zaidi ya miaka 50,historia binafsi kama umewahi kuwa na saratani ya matiti,historia ya familia kuwa na ndugu upande mama aliyewahi kuwa na saratani ya matiti, kurithi vinasaba vyenye hitilafu kutoka kwa wazazi.
Pia kuanza hedhi mapema chini ya umri wa miaka 12,kuchelewa kukoma hedhi baada ya miaka 55,kuchelewa kupata mtoto wa kwanza baada ya umri wa zaidi ya miaka 30,kutowahi kabisa kubeba mimba na kutonyonyesha.
Vihatarishi vya saratani ya matiti vinavyoweza kuzuilika
Anaekeza kuwa vihatarishi vinavyoweza kuzuilika ni pamoja na kutokufanya mazoezi, hivyo kuwa na unene uliokithiri (obesity),matiti kupata mionzi wakati wa tiba ya mionzi,unywaji wa pombe uliokithiri,ulaji wa vyakula vyenye mafuta haswa yatokanayo na wanyama,kutokutumia mboga mboga na matunda kwa wingi pamoja na kutokunyonyesha mtoto zaidi ya miaka miwili.
Uchunguzi wa saratani ya matiti
Dkt.Ngabakubi anaeleza kuwa inashauriwa kufanya uchuguzi wa awali kabla ya kuona dalili zozote pia mwanamke ambaye bado anapata hedhi anapaswa kujichunguza matiti siku ya tano baada ya kumaliza hedhi huku mwanamke ambaye amekoma hedhi anachagua siku yoyote katika mwezi ya kujifanyia uchunguzi.
Jinsi ya kujichunguza saratani ya matiti
Aidha Dkt.Ngabakubi anaeleza kuwa
mwanamke huweza kujichunguza mwenyewe akiwa anaoga au amekwishaoga kwa kusimama mbele ya kioo au akiwa amelala na kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuweka mikono chini, juu, au kiunoni na kuangalia rangi, ukubwa wa matiti na kulinganisha la kushoto na lile la kulia.
Pia kiganja cha kushoto kitapima titi la kulia na kiganja cha kulia kitapima la kushoto kwa kuzunguka ziwa lote,kisha atapima kwenye chuchu na kukamua kuona kama linatoa majimaji au damu na mwisho ataangalia kama tezi za kwapani zimevimba.
Ugunduzi wa saratani ya matiti
Anaeleza kuwa ili ugundue kama una saratani vipo baadhi ya vipimo ambavyo vinatumika kwa ajili ya kufanyabuchunguzi na kugundua kama mtu ana saratani ya matiti ikiwemo Ultrasound ambacho ni kipimo kinachotumika kuangalia viungo ndani ya mwili.
Pia Fine Needle Aspiration Cytology-(FNAC)kutoa kipimo cha majimaji ndani ya kivimbe kwa ajili ya kupima kwenye darubini,Biopsy ni kipimo cha maabara cha kuangalia kinyama kilichokatwa kutoka kwenye titi au majimaji kuhakiki saratani ya matiti.
Pamoja na vipimo vya picha kama mammography, X-ray, ultrasound, CT scan, MRI na PET scan huweza kufanyika kuchunguza dalili na hatua ya saratani ilipofikia.
Tiba ya saratani ya matiti
Anaeleza kuwa kutegemea hatua saratani ilipofikia na hali ya kiafya ya mgonjwa, mgonjwa anaweza kupatiwa tiba ya upasuaji, tiba ya kemia, tiba ya mionzi, tiba ya kibaiolojia na tiba shufaa ambapo tiba hizo huweza kutolewa moja au zaidi ili kuongeza mafanikio ya matibabu.
Kinga ya saratani ya matiti
Dkt.Ngabakubi,anaeleza kuwa japo
saratani ya matiti haiwezi kuzuilika moja kwa moja, uwezekano wa kupata saratani huweza kupunguzwa kwa kufanya mambo mbalimbali ikiwemo kuishi mtido bora wa maisha kwa kula chakula kinachofaa kama mboga mboga za majani na matunda, kupunguza ulaji wa mafuta haswa ya wanyama, kuacha matumizi ya tumbaku na kupunguza unywaji wa pombe uliokithiri, kufanya mazoezi na kupunguza unene.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia