January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Asante ya Sadio Mane ni Hospitali kule alipozaliwa

Na Philemon Muhanuzi

ILIMCHUKUA Sadio Mane dakika mbili na sekunde hamsini na sita kufunga magoli matatu na kuweka historia mpya katika ligi kuu ya Uingereza.

Mechi kati ya Southampton dhidi ya Aston Villa iliyochezwa May 2015 ilimalizika kwa magoli 6-1 na Mane kuifungia Southampton magoli hayo matatu ya kibabe.

Jurgen Klopp kocha mkuu wa Liverpool hakuhitaji tena ushahidi wa ubora wa upambanaji wa mshambuliaji huyo ambaye ni raia wa Senegal.

Mane hana urefu kama wa washambuliaji wengi wa kati, umbo lake la kawaida tu lakini anao mwili wenye nguvu za asili za kiafrika.

Hahitaji sana mipira ya hewani kama kina Olivier Giroud, Emmanuel Adebayor na wafungaji wengine maarufu.

Anahitaji aburuziwe pasi kutoka kwa viungo wachezeshaji na mabeki ili aanze kuwafuata mabeki na kuwapunguza. Wenye kuvifahamu vionjo vya kweli vya mshambuliaji siku zote wanamkubali sana Mane.

Wapo wenye kuamini kwamba Lionel Messi alipewa tuzo ya sita ya mwanasoka bora wa dunia, akibebwa na siasa za makampuni makubwa yenye kufanya nae biashara ya matangazo ya bidhaa.

Kwamba ilifanyika mizengwe ya kiutu uzima ndipo Lionel Messi akapewa tuzo, wakati katika soka la ligi ya mabingwa Barcelona walifungwa na Liverpool magoli manne katika mechi ya marudiano na hakuna cha maana alichofanya Messi.

Wapenda soka hao wanaamini kwamba kama sio Sadio Mane basi Mohamed Salah ndio washindi wa tuzo hiyo waliyonyang’anywa haki yao.

Wanaamini katika zile siasa za mwanasoka kutoka Afrika kupewa ushirikiano wakati anatazamwa machoni lakini akigeuka na kuondoka anaanza kudharauliwa.

Katika siku hizi ambazo dunia nzima biashara maarufu ni ile ya barakoa, wapenda soka wamekumbushwa juu ya moyo wa upendo.

Moyo wa utu kwani mzima wa leo ndio mgonjwa wa uhakika wa kesho asubuhi. Kila mwanasoka anataka aonekane akigawa chakula katika mitaa yenye nyumba wanazoishi wazee na watu wa kundi maalum kiafya.

Kila mtu maarufu anakuwa ni habari ya ukurasa wa kwanza yenye kuhusiana na tendo zito la upendo kwa jamii ya walio wengi.

Sadio Mane amekuwa ni sehemu ya huruma ya wanamichezo ambayo imekuwa kubwa mwanzoni mwa mwaka huu mzito wa janga la corona.

Mane anajenga hospitali huko kwao Senegal ili iwatibu na iokoe afya za wanakijiji wa sehemu aliyozaliwa na kukulia.

Waingereza wanao ule utamaduni wa kurudisha sehemu ya upatacho kwa jamii inayokuzunguka, wenyewe wanaita Corporate Social Responsibility (CSR).

Mane mwenye kulipwa mshahara wa Paundi laki moja kwa wiki, haoni mantiki ya kuishi maisha yenye mbwembwe nyingi za magari wakati kijijini kwao cha muhimu ni ujenzi wa Hospitali kubwa.

Yeye mwenyewe anasema alitembea kwa miguu kwenda uwanja wa mazoezi na kurudi nyumbani. Miiba ilikuwa ya kwake, mawe ya viwanja vibovu yalikuwa ya kwake, michubuko ya pembeni ya mapaja ilikuwa ya kwake.

Mapito yake mpaka kufikia kucheza soka la Ulaya, hayakuwa ni yale yenye kufanana na namna wafalme wanavyowekewa mazuria mekundu ili wasichafuke. Anajisikia vibaya kila anapokumbuka umaskini aliouacha kule alipozaliwa.

Kama anao uhakika wa kuishi vizuri leo hii na kesho kwanini asitafute Baraka za Mungu kwa kujenga Hospitali itakayoleta mabadiliko chanya ya kiafya kule nyumbani kwao?.

Inaweza kuwa vigumu kwake kuwanunulia viatu wanavijiji wote, inaweza kuwa vigumu kuwajengea nyumba za kisasa wanakijiji wote, lakini Hospitali itawagusa wote kwa namna njema zaidi.

Mane anajiwekea kingo za ulinzi wa Mungu,ambazo hazibomolewi na chuki au fitina ya kibinadamu.

Ni Mane huyu huyu anayekuta wafanyakazi wakishusha maji ya kunywa ya chupa za plastiki kutoka kwenye gari na yeye anasaidia kubeba pasipo kupita pembeni kama vile hawaoni.

Hana makuu, hana ulimbukeni wa kulipizia maisha ya kimaskini aliyoishi utotoni. Anarudisha asante nzito sana kwa kujenga hospitali itakayotumika kwa faida ya sehemu aliyozaliwa.

Ameshafanikiwa tayari kwa kubeba kombe la ligi ya mabingwa Ulaya mwaka jana, lakini kwa Baraka za Hospitali sitashangaa siku moja akibeba tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Amekuwa ni mtu anayepanda wema, na huwa hauna sifa ya kuoza.