Na Munir Shemweta, WANMM
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameanza kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za ardhi katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Akiwa njiani akitokea mkoani Morogoro katika ziara yake hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa Dumila wilayani Kilosa walimueleza kuwa maeneo yao yana migogoro mingi ya ardhi jambo walilolieleza linalosababisha kushindwa kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.
Dkt.Mabula alianza utekelezaji maagizo hayo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya kikao cha ndani na viongozi wa wilaya ya Kilosa wakiwemo wenyeviti wa vijiji, watendaji wa mitaa, madiwani pamoja na wananchi waliowasilisha malalamiko kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan.
Wakati wa kikao hicho, wenyeviti wa mitaa wakiongozwa na madiwani walieleza migogoro ya ardhi katika maeneo yao kuwa ni ile ya mipaka kati ya vijiji, kubomolewa kwa baadhi ya nyumba za wananchi, kutopimwa baadhi ya vijiji, wananchi kuzuiwa kuendelea na shughuli za kiuchumi na wanaodaiwa wamiliki halali pamoja na mgogoro ya uvamizi wa maeneo.
Akizungumza na viongozi hao tarehe 12 Julai 2021 wilayani Kilosa, Dkt Mabula alieleza kuwa, migogoro mingi ya ardhi imesababishwa na wenyeviti wa vijiji hasa katika suala la ugawaji ardhi na kusisitiza kuwa mwenye mamlaka ya kugawa ardhi ya kijiji ni mkutano wa kijiji na siyo mwenyekiti wa kijiji na ardhi hiyo haitakiwi kuzidi ekari 50.
“Kasimamieni vizuri vijiji vyenu na mhakikishe ardhi katika maeneo yenu inapimwa na kupangwa maana itapunguza migogoro ya ardhi katika maeneo yenu,”amesema.
Akieleza suala la migogoro ya mipaka, Dkt Mabula alisema, suala la kupima mipaka ni la halmashauri kwa kutenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo na kuhakikisha vijiji vinapimwa na kupatiwa vyeti na alitaka utengaji fedha ufanyike kila mwaka.
“Sisi kama Wizara hatuna wajibu wa kupima mipaka ya vijiji, madiwani mtekekeze majukumu yenu kwa kusimamia upimaji vijiji na msipotekekeza kilosa haitakaa itulie na RAS aunde timu yake chini ya usimamizi wa mpima wa mkoa na kuweka kambi vinginevyo hatuwezi kufika,” amesema Dkt.Mabula.
Kuhusu ufutaji mashamba, Naibu Waziri wa Ardhi alisema, katika upangaji wa mashamba yaliyofutwa serikali inazingatia uhitaji wa wakulima, wafugaji pamoja na uwekezaji hivyo mashamba yanaporudishwa kwa wananchi mpango wa matumizi kwa ajili ya shughuli mbalimbali unazingatiwa kulingana na mahitaji yaliyopo ambapo alisisitiza kuwa mashamba hayo hayarudishwi kwa wananchi pekee.
Aidha, alisisitiza kwa kuwaeleza viongozi hao kuwa, suala la kuvamia mashamba na kukaa miaka 30 haijengi uhalali mwananch kujiona mmiliki halali na kuongeza kuwa, kutokana na serikali kuwajali wananchi wake ndiyo maana inawafikiria waliovamia kwa kuwaachia sehemu ya mashamba.
Kwa upande wake Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Mizikunte akizungumza katika kikao hicho aliwataka wananchi kuheshimu mhimili wa mahakama pale unapotoa maamuzi kuhusiana na migogoro ya ardhi na kusisitiza kuwa hakuna namna ya kukwepa maamuzi hayo.
Kuhusu mashamba, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro aliishukuru serikali kwa kuujali mkoa huo ambapo alisema katika kuhakikisha mashamba yanapimwa mkoa umetengewa fedha kwa ajili ya kupima jumla ya mashamba 15 katika wilaya hiyo.
Wilaya ya Kilosa imekuwa na migogoro ya ardhi kwa muda mrefu ikiwemo migogoro iliyohusisha wawekezaji wa mashamba makubwa walioshindwa kuendeleza kwa mujibu wa sheria jambo lililosababisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kufuta jumla ya mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 katika wilaya hiyo ili kugawiwa kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na uwekezaji.
Aidha, Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia pia ufufuaji wa mashamba 49 yenye ukubwa wa ekari 45,788.5 yaliyotaifishwa miaka ya nyuma huku na wananchi wakiwa hawana uhakika nayo ambapo Mhe. Rais ameelekeza sehemu kubwa ya mashamba hayo kutumiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo.
More Stories
Tanzania,Uturuki kushirikiana kuinua sekta ya utalii nchini
Wanaoficha watoto wenye ulemavu kusakwa
Mawakili Tabora walaani kuziwa kutekeleza majukumu