April 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aliyekiri kulawiti afungwa jela maisha

Na Jumbe Ismailly TimesMajira Online, Singida

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Singida imemuhukumu adhabu ya kutumikia kifungo cha maisha jela mkazi wa Mtaa wa Minga katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Husein Azizi (34) baada ya kukiri kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka minne.

Mwanasheria wa serikali, Elizabeth Barabara amedai kuwa, mshitakiwa alitenda kosa la kumlawiti mtoto mwenye umri wa miaka minne Agosti 6, 2020 Mtaa wa Minga.

Baada ya kusomewa shitaka lake, mshtakiwa huyo amekiri na kudai hakuwa akifanya kitendo hicho kwa mtoto huyo peke yake bali kulikuwa na mtoto mwingine ambaye aliyefanyanae kitendo hicho bila kugundulika.

Kwa mujibu wa mwanasheria huyo, mshitakiwa Azizi amedai, watoto hao walikuwa wakimfuata hadi machungani kutokana na kuwa walimpenda sana na hakuwa amefanya tendo hilo mara moja bali alikuwa akifanya mara kwa mara.

Hata hivyo Elizabeth amedai, baada ya mshitakiwa huyo kukiri kosa lake na kutiwa hatiani na Mahakama hiyo, amewasilisha utetezi wake kwa kuomba msamaha na kuahidi kwamba hatarudia tena kufanya kitendo kama hicho.

Katika utetezi wake mwingine, mshitakaiwa huyo amekiri kitendo alichokifanya kwa watoto hao wawili hakikuwa kizuri na hivyo kuomba Mahakama hiyo imuonee huruma na kumpa adhabu ndogo.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo ya jinai namba 135/2020, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Robert Oguda amesema ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya mshitakiwa huyo, atahukumiwa kwenda kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha jela.