Na Penina Malundo,timesmajira,online
WATU wenye Ualbino Mkoa wa Dar es Salaam, waiomba Serikali kuwapatia mafuta yanayosaidia kukinga Ngozi dhidi ya mionzi ya jua ambapo mara ya mwisho Serikali iliwapatia mafuta hayo mwaka 2017.
Pia wamesema ukosekanaji wa mafuta hayo unawafanya kuweza kupata athari za ngozi kutokana na ngozi zao kupigwa na jua.
Hayo yalisemwa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Mkoa wa Dar es Salaam, Gabriel Aruga. Amesema tangu walipopatiwa mafuta hayo mwaka 2015 na Serikali hadi sasa hawajawahi kupatiwa licha ya Serikali kuingiza katika mpango wake wa kutoa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Amesema mafuta wanayoyapata kwa sasa ni yale yanayotolewa na wahisani au wadau ndiyo wanayotumia, ambapo nayo ni machache hayawakidhi wote kwa idadi yao.
Aruga alisema mafuta ya ngozi kwa watu wenye ualbino ni muhimu, kwani usaidia kuimarisha ngozi zao hivyo wanapokosa mafuta hayo usababisha ngozi kuuma na wakati mwingine upelekea kupata saratani
“Kwa Mkoa wa Dar es Salaam tupo wanachama kama 1,000 ambao tunatambulika ila katika kupatiwa mafuta kinga mwaka 2015 tuliopewa na serikali chubu 700 ambapo kila mmoja alipata chubu tatu,”amesema na kuongeza;
“Mwanzoni Serikali ilisema mafuta hayo yameingizwa katika bajeti ya dawa za MSD, lakini tangu kipindi hicho hadi sasa hatujawahi kupatiwa zaidi ya wadau wengine kutusaidia.”
Kwa upande wake mmoja wa wanachama wa Mkoa wa Dar es Salaam,Joyce Maige alisema mwaka 2015 ndipo alipofanikiwa kupata mafuta ya ngozi ambayo yalitolewa na Serikali na kufanikiwa kupata vichupa viwili.
Amesema baada ya hapo hakuweza kupata tena mafuta hayo hali ambayo baadae ilimpelekea kupata kupata vipele na kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu.
“Nilipopata vipele usoni nikaenda Hospitali ya Temeke ambapo nilipewa rufaa kwenda Hospitali ya Mwananyamala na huko ndipo nilipopata matibabu na kupewa mafuta mengine ambayo yalinisaidia,”alisema
Alisema ukosefu wa mafuta ya ngozi kwa Albino inawafanya watu wa Albino kupata shida hususani pindi jua linapowaka nyakati za mchana na kufanya ngozi kuuma.
“Kwa sasa tunawashukuru wafadhili mbalimbali ambao wao ndio wanaotupatia haya mafuta (sun skin) ila mafuta wanayoyatoa bado hayatukidhi mahitaji yetu kwa sababu tupo albino wengi,”amesema
Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,(TAMISEMI),Rashid Maftaa, amesema Wizara ya Afya ilitoa katoni 30,000 ya mafuta hayo kwenye mpango wa MSD kwa ajili ya vituo vya afya.
Alisema Ofisi yao ya Tamisemi tayari iliwaelekeza Katibu tawala wa Mikoa kuelekeza wakurugenzi wa Halmashauri kuelekeza vituo vya afya na zahanati kuagiza mafuta hayo kwa MSD kwani yanapatikana huko.
“Mwaka huu wa fedha,Wakuu wa Mikoa waelekeze wafamasia wa mikoa na halmashauri kujumuisha mchakato wa uandaaji wa maksio ya mahitaji ya Dawa ,Vifaa na vifaa tiba kwa mwaka ujao wa fedha ambapo zoezi hili tayari limeanza kwa lengo la kujua idadi kamili inayohitajika ya mafuta kwa watu wenye ualbino,”Amesema
More Stories
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari