Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Kilindi
WAJUMBE wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Tanga wametaka kasoro zilizojitokeza katika mradi wa ujenzi unaoendelea katika Hospitali ya Wilaya ya Kilindi zirekebishwe.
Wakizungumza Februari 28, 2024 kwenye majumuisho mara baada ya ukaguzi wa miradi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi, wamesema thamani ya fedha imeonekana, na hata ujenzi wenyewe, bali kasoro ndogo ndogo zipo kwenye maeneo kama milango baadhi ina mianya.
“Tunataka mtu yeyote atakaekuja kukagua aweze kwenda sambamba kwa kuona kile tulichokiona sisi,tunataka kasoro tulizoziona zirekebishwe kabla ya watu wengine hawajafika” amesema Diwani wa Kata ya Kwamatuku, Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mustapha Beleko.
Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga Erasto Mhina ,ameagiza nyaraka za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi ziwekwe sehemu moja ili mtu ama taasisi yeyote inapotaka kukagua zipatikane kwa urahisi.
Pia ametaka ubora wa vifaa vya ujenzi ikiwemo mabati uendelee kuzingatiwa kwenye miradi ya Serikali.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi Dkt. Elizabeth Washa amesema hadi sasa hospitali hiyo imepokea kiasi cha bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo mbalimbali.
“Kwa mwaka wa fedha 2020/2021 mnamo Novemba 16, 2021, halmashauri ilipokea fedha za UVIKO 19 kwa awamu ya kwanza milioni 390 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la dharura (EMD) na nyumba ya watumishi (3-1),”ameeleza na kuongeza:
“Ujenzi wa nyumba umekamilika na inatumika, ambapo ujenzi wa jengo la dharura umebakia ufitishaji wa mifumo ya gesi kwa ajili ya wagonjwa mahututi huku kiasi cha milioni 1.2 kimesalia kama fedha ya angalizo kwa kazi zilizosalia.
Pia ameeleza kuwa Januari 27, 2022 halmashauri ilipokea fedha awamu ya pili kutoka Serikali Kuu kiasi cha milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya wagonjwa wa nje na maabara,utekelezaji wake ulianza Mei 2022.
Katika utekelezaji huo, jengo la maabara limetumia kiasi cha milioni 130 na jengo la wagonjwa milioni 370 huku kiasi cha milioni 5.2 kimesalia kama fedha ya angalizo kwa kazi zilizofanyika kwa kipindi kisichozidi miezi sita.
Dkt. Washa amesema halmashauri kupitia vikao halali, iliongeza kiasi cha milioni 40 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la wagonjwa wa nje.
Pia mwaka wa fedha 2022/2023 walipokea kiasi cha milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya jengo la wazazi (combined maternity complex) hadi sasa kiasi cha milioni 475 zimetumika na jengo lipo hatua za ukamilishaji wa madirisha na milango.
Amesema Oktoba 27, 2023 walipokea kiasi cha milioni 500 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali ya wilaya,fedha hizo zimeelekezwa kutekeleza ujenzi wa jengo la mionzi (X- ray na Ultrasound), jengo la dawa (pharmacy), jengo la kufulia na kichomea taka.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Korogwe Francis Komba, amesema jengo la dharura limejengwa kwa ubora wa hali ya juu huku likionesha kuwa kubwa zaidi na vyumba vingi tofauti na majengo mengine kwenye halmashauri nyingine.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Faraja Msigwa amesema Hospitali ya Wilaya ya Kilindi imefunguliwa Februari 23, 2024 kwa kuanza kutoa huduma ya wagonjwa wa nje na huduma za mama na mtoto (RCH).
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia