May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ACP. Muliro Jumanne

Ajali yaua watu 8 na kujeruhi 5

Na Daud Magesa, TimesMajira Online, Mwanza

WATU nane wamefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa katika ajali iliyosababishwa na magari mawili na trekta moja kugongana katika Kijiji cha Ihayabuyaga, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema ajali hiyo imetokea jana Juni 10, saa 1:45 jioni katika Kijiji Cha Ihayabuyaga, Kata ya Bukandwe, Wilaya ya Magu katika barabara kuu ya Mwanza-Musoma.

Amesema, kutokana na ajali hiyo, watatu 8 wamefariki papo hapo akiwemo dereva wa gari dogo la abiria na wengine watano kujeruhiwa huku jeshi hilo likimshikilia dereva wa Lori lililobababisha ajali hiyo, Boniface Cliford ‘Tuju’ (37) mkazi wa Nera.

Akielezea tukio hilo, Muliro amesema, wakati Tuju akiendesha lori hilo lenye namba T 322 DCB aina ya Scania mali ya Texas Hardware, likiwa na tela namba T 1351 DCA akitokea Wilayani Busega kwenda Mwanza, baada ya kufika Ihayabuyaga aliligonga trekta ambalo halikuwa na taa za nyuma na kupoteza mwelekeo.

Baada ya kuligonga trekta hilo lenye namba T 952 DGW, nalo liligonga gari ya abiria iliyokuwa ikitoka Mwanza kwenda Magu, aina ya Nissan Hiace yenye namba T 775 DEG mali ya George Philipo Msangi ambaye alikuwa akiiendesha na kusababisha abiria nane kupoteza maisha na watano kujerihiwa.

Majeruhi wanne waliokimbizwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Mwanza (BMC) ni Mratibu Elimu Kata ya Chabula , Ayubu Mindule, Edibini Makubo (20) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika Sekondari ya Bariadi High na Elias Lutandula (46), wote wakazi wa Kijiji cha Nyanguge na Kasabuku Kishela (32), mkazi wa Magu huku Elias Francis (44) mkazi wa Nyangug akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Magu kwa matibabu na kwamba hali zao zinaendelea vizuri.

Kamanda Murilo amesema, marehemu waliotambuliwa hadi sasa ni wawili ambao ni dereva wa Nissan, George Msangi, mkazi wa Magu na mwalimu wa Shule ya Sekondari Lugeye, Hamis Masige (35),mkazi wa Lugeye ambapo miili ya marehemu wengine 6 bado haijatambuliwa.

Amesema, mbali na kumshikilia dereva wa lori pia Jeshi hilo linamsaka dereva wa trekta hilo ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria kwani mara baada ya ajali kutokea alikimbia.