May 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aina tatu mpya za kahawa yaTanzania zazinduliwa Japan

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Kampuni ya ITO EN LTD, ambayo ni kampuni tanzu ya Tully’s Co. Ltd., inayomiliki migahawa maarufu ya Tully’s Coffee, imezindua aina tatu mpya za kahawa ya Tanzania, nchini Japan katika hafla iliyofayika jijini Tokyo tarehe 14 Machi, 2024. 

Aina za kinywaji hicho pendwa nchini humo kinachotokana na  kahawa kutoka Tanzania ni TULLY’s COFFEE BARISTA BLACK KILIMANJARO; TULLY’S COFFEE MY HOME BLACK KILIMANJARO; na TULLY’S COFFEE BARISTA ROAST COLD BREW – KILIMANJARO BLEND. Kahawa hizo ni kutoka mkoa wa Arusha, Tarime mkoani mara na mashamba ya GDM yaliyoko Mbozi mkoani Mbeya. 

Zoezi hilo la uzinduzi lililofanyika katika Ubalozi wa Tanzania jijini Tokyo na liliongozwa na Mhe. Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan, lilimshirikisha pia Bw. Osamu Aizawa, Meneja Mkuu wa Kampuni ya ITO ENaliyeambatana na wawakilishi wa kampuni hiyo na Kampuni ya Tully’s Coffee.

Kampuni ya ITO EN Ltd. ambayo, ni kampuni tanzu ya Tully’s Coffee ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya vinywaji nchini Japan, inamiliki migahawa ya kahawa takriban 700 nchini humo huku ikiwa imejipatia umaarufu mkubwa katika biashara ya uuzaji wa kahawa aina mbalimbali duniani. 

Hii ni mara ya pili, kwa Kampuni ya Tully’s kuzindua kahawa ya Tanzania katika migahawa yake, uzinduzi kama huu uliwahi kufanyika  mwezi Juni na Agosti 2023 ukihusisha kahawa aina ya GDM full washed, GDM natural na Tarime Coffee.

Kuzinduliwa kwa aina nyingine tatu mpya za kahawa nchini Japan, kunaendelea kuleta uhakika na kuongezeka kwa soko la kahawa ya Tanzania nchini Japan ambayo imejizolea umaarufu mkubwa kwa ubora na ladha ya aina yake na kupelekea kupewa jina maarufu la kibiashara la Kilimanjaro Coffee.

 Kilimanjrao Coffee ni miongoni mwa bidhaa tatu za kahawa zinazopendwa zaidi Japan;na jina hilo hutumika nchini humo kwa kahawa zinazozalishwa Tanzania pekee, kwa kutambua kivutio kikubwa cha Mlima Kilimanjaro uliopo nchini Tanzania. 

Tanzania inasifika Japan kwa kuzalisha kahawa bora aina ya Arabica (Arabica laini – full washed na Arabica ngumu – natural) inayolimwa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Njombe, Iringa, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kigoma, Songwe na Mbeya; na kahawa ya Robusta inayolimwa mkoani Kagera. 

Akizungumza katika uzinduzi huo, Balozi Baraka Luvanda alizihakikishia kampuni za Japan, uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wanapoamua kuwekeza katika kilimo au sekta nyinginezo hapa nchini. 

Balozi Luvanda amelitaja zao la kahawa kuwa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati yanayongoza kwa kulipatia Taifa pato na kuingiza fedha za kigeni. Akitolea mfano wa Japan, alieleza kuwa kwa mwaka, Tanzania inauza kahawa yake Japan kwa wastani wa asilimia 33 ya kahawa inayolimwa nchini, ambayo ni sawa na wastani wa kilogramu million 15 (tani 15,000) ya kahawa yote ya Tanzania inayouzwa nchini humo. Takwimu zinazoifanya Japan kuwa mnunuzi  namba moja (1) wa kahawa inayolimwa nchini.

Aidha, Balozi Luvanda alielezea juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika miradi ya muda mrefu na mfupi ikiwemo kutatua changamoto za kilimo kuanzia shambani hadi sokoni ili kujihakikishia uhakika wa chakula na biashara.  

Vilevile Balozi ametoa wito kwa wadau wa kahawa nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Maonesho ya Kimataifa ya Kahawa ya Mwaka 2024 (World Specialty Coffee Conference and Exhibition 2024) yanayotarajiwa kufanyika jijini Tokyo mwezi Oktoba 2024, ambayo yanaratibiwa na Ubalozi kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania.