May 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ahukumiwa kunyongwa baada ya kumuua mtoto wake

Esther Macha, Timesmajira, Online, Mbeya

MKAZI wa mji Mwema wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Geofrey Emilio (25)amehukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya mtoto wake wa kumzaa mwenye umri wa miezi mitano ikidaiwa kuwa ni migogoro na wivu wa kimapenzi kati yake na mkewe.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu mkazi mkuu katika mahakama ya hakimu mkazi Mbeya, Paul Ntumo mwenye mamlaka ya nyongeza kutoka mahakama kuu kusikiliza kesi za mauaji, baada ya mahakama kuridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka kupitia mashahidi wasiopungua wanne akiwemo mama wa mtoto bila kuacha shaka yoyote.

Akisoma hukumu hiyo hakimu Ntumo amemtaja mshtakiwa kuwa ni Geofrey Emilio Mwagongo kijana wa miaka 25 ambaye baada ya kuanza maisha ya ndoa na mkewe miaka michache iliyopita anadaiwa alikuwa na mwanamke mwingine ambaye katika mawasiliano alimtumia ujumbe kujua ikiwa anampenda na yupo tayari kuishi naye na watoto wake ujumbe ambao mke wake aliuona na kuwa mwanzo wa mgogoro baina yao.

Hakimu huyo amesema katika ushahidi wa jamhuri uliowasilishwa mbele yake ameridhika nao kwamba ni kweli mshtakiwa kwa makusudi na kwa nia ovu alimuua mtoto wake kikatili kwani ushahidi hususani wa mama mzazi wa mtoto, jeshi na polisi na taarifa za uchunguzi wa kidaktari ulionyesha kwamba mzazi huyo alimzika mtoto huyo akiwa hai.

Amesema shahidi namba moja wa jamhuri aliieleza mahakama kwamba siku ya tukio Agosti 28, 2018 majira ya asubuhi mumewe alimuomba ampatie mtoto wao ili akatembee naye lakini hakurudi naye hadi majira ya jioni ndipo alianza kutafutwa lakini baada ya kurudi nyumbani baba huyo alidai mtoto huyo amempeleka nyumbani kwao Iringa ambako baada ya kupiga simu waliambiwa hakuna mtoto, baadaye alidai amempeleka Igurusi wilayani humo (Mbarali) wakati sio kweli.

Katika kurejea huko kwa ushahidi wa jamuhuri katika kesi hiyo namba 07/2020 mahakama inasema baada ya mshtakiwa kulazimishwa aeleze alikompeleka mtoto ndipo alipowataka maafisa wa polisi kwenda naye ili akawaonyeshe ambapo walienda katika pori moja huko Uwanji na kuonyesha eneo ambalo alimfukia mtoto wake huyo akiwa hai taarifa zikieleza kwamba ni baada ya kumnywesha mchanganyiko wa juisi na maji ya betri bila lakini hakufariki dunia.

Baada ya polisi kufukua mwili wa marehemu mtoto, Princes Geofrey Mwagongo na kwenda hospitali kwa uchunguzi zaidi ambapo akitoa utetezi wake mshtakiwa alidai kutenda kosa hilo kwakuwa alichanganyikiwa kutokana na wivu wa kimapenzi na mgogoro wa kati yake na mkewe hivyo kuiomba mahakama kumsamehe.

Kabla ya mahakama kutoa maamuzi, Mwendesha mashtaka wa serikali wakili Davice Msanga aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na jamii kwa ujumla kutokana na watu kuendekeza hasira zisizo na maana na kudhuru maisha ya watu wengine na kukatisha ndoto zao.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu mkazi mkuu katika mahakama ya hakimu mkazi Mbeya mwenye mamlaka ya nyongeza kusikiliza mashauri ya mauaji Paul D. Ntumo amemhukumu kijana Geofrey Mwagongo (25) adhabu ya kunyongwa hata kufa kwa kosa hilo na kuweka wazi haki ya kukata rufaa kwa asiyeridhika na maamuzi hayo ya mahakama kuu Mbeya.