Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
TAASISI ya Aids Healthcare Foundation (AHF) nchini imesema inatumia uwezeshaji wa kiuchumi kwa makundi yaliyo katika hatari ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kama sehemu ya juhudi za kupunguza maambukizi mapya na kuwawezesha kujitegemea.
Akizungumza kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo, Dkt. Maige Charles wa AHF amesema kuwa baadhi ya watu hujikuta katika mazingira hatarishi kutokana na changamoto za kiuchumi, ikiwemo kukosa kipato na mahitaji muhimu kama chakula.
Amesema kupitia miradi ya uwezeshaji, ikiwemo Girls Act na Isuto Men, AHF huwafikia watu hao kwa kushirikiana na wenzao wanaofahamu mazingira na changamoto zinazowakabili, ili kuwasaidia kupata ujuzi wa kuwawezesha kujipatia kipato.
Kwa mujibu wa Dkt. Maige, walengwa hukusanywa katika vituo vya rasilimali (resource centres), ambako hupewa nafasi ya kuchagua ujuzi wanaotaka kujifunza kulingana na mahitaji na malengo yao. Baadhi huchagua kujifunza ususi, utengenezaji wa sabuni au ufundi wa kunyoa nywele ili waweze kujiajiri.
Amesema vituo hivyo hushirikiana na wakufunzi kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), ambao huwafundisha walengwa kwa kutumia vifaa vinavyopatikana katika vituo hivyo. Baada ya kukamilisha mafunzo, wahitimu huingia katika shughuli za uzalishaji na kujipatia kipato, huku kundi jingine likipatiwa nafasi ya kunufaika na mpango huo.

Katika eneo la kinga dhidi ya VVU, Dkt. Maige amesema AHF inaunga mkono utoaji wa kondomu, dawa za kinga kabla ya uwezekano wa kuambukizwa VVU (PrEP) na dawa za kinga baada ya uwezekano wa kuambukizwa (PEP), ili kuongeza fursa za watu kujikinga na maambukizi.
Aidha, amesema taasisi hiyo inashirikiana na Serikali kuimarisha huduma za matibabu kwa kusaidia upatikanaji wa baadhi ya vifaa tiba, huduma za maabara, upimaji na huduma katika vituo vya huduma na tiba kwa watu wanaoishi na VVU (CTC). Pia, husaidia upatikanaji wa dawa za kutibu magonjwa nyemelezi.
Ameongeza kuwa AHF inafanya juhudi za kuwafikia watu ambao hawapati huduma kwa urahisi, hasa wanaume na wanaoishi katika maeneo ya mbali, migodi na maeneo ya uvuvi.
Amesema baadhi ya makundi hayo huwa na changamoto ya kufika hospitalini kutokana na gharama za usafiri, muda na ratiba zao za kazi, hivyo wahudumu hulazimika kuwafuata walipo, wakati mwingine nyakati za usiku, kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

More Stories
CRDB yavutiwa na ubunifu wa vijana VETA, yatoa zawadi
Mkenda: Tuamini wataalamu wetu, tupunguze utegemezi wa Nje
VETA yafungua milango ya mafanikio kwa wenye ulemavu