Na Joyce Kasiki
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete, ametangaza maandalizi ya Mkutano Mkuu wa 11 wa Mwaka wa Mtandao wa Wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Barani Afrika (APS-HRMnet), utakaofanyika Novemba 10 hadi 13, 2026, katika Ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar, na unatarajiwa kukutanisha washiriki takribani 800.
Kwa mujibi wa taarifa ya Waziri huyo ,hadi Oktoba 9, 2026, washiriki 404 kutoka nchi 11 walikuwa wamejisajili na kuthibitisha kushiriki mkutano huo. Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Nigeria, Sierra Leone, Côte d’Ivoire, Ghana, Namibia, Lesotho na Zimbabwe.
Mkutano huo utatumia kaulimbiu isemayo, “Kuwezesha Mabadiliko ya Kimkakati ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Afrika kwa Kutumia Akili Unde,” ikiwa na lengo la kuhimiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kuboresha usimamizi wa watumishi na utoaji wa huduma kwa umma.
Taarifa hiyo imesema ,mkutano huo unalenga kuwakutanisha viongozi, wasimamizi wa rasilimaliwatu, wanataaluma na wataalamu wa utumishi wa umma kutoka nchi mbalimbali za Afrika ili kujadili mikakati madhubuti ya mageuzi ya rasilimaliwatu yatakayoongeza tija na kuboresha utendaji katika sekta ya umma.
Aidha imesema,washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu na utaalamu kuhusu matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence) katika usimamizi wa rasilimaliwatu, kuboresha mifumo ya kiutendaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Taatifa hiyo imesema uongozi mbalimbali wa Afrika wamethibitisha kushiriki mkutano huo, wakiwemo Waziri na Katibu Mkuu wa Sierra Leone, Katibu Mkuu wa Somalia, Katibu Mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Katibu Mkuu wa Guinea-Bissau, Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu wa Kenya, pamoja na Katibu Mkuu wa Zambia.
Mtandao wa APS-HRMnet unajumuisha nchi za Afrika zilizogawanyika katika kanda tano, ambazo ni Afrika Magharibi yenye nchi 17, Afrika Mashariki nchi 10, Afrika ya Kati nchi nane, Afrika Kaskazini nchi sita na Kusini mwa Afrika nchi 13. Mtandao huo unalenga kutafsiri mikakati ya maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa ili kujenga rasilimaliwatu yenye uwezo wa kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Tanzania, ikiwa mwanachama wa APS-HRMnet na mwenyeji wa mkutano huo, inatarajiwa kutumia fursa hiyo kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika maendeleo ya rasilimaliwatu.
Washiriki pia watapata nafasi ya kujifunza tamaduni za Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na kufahamu mchango wa Watanzania katika kudumisha amani, utulivu, umoja na ushirikiano.

More Stories
AHF yatumia uwezeshaji kupunguza VVU
CRDB yavutiwa na ubunifu wa vijana VETA, yatoa zawadi
Mkenda: Tuamini wataalamu wetu, tupunguze utegemezi wa Nje