October 9, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRDB yavutiwa na ubunifu wa vijana VETA, yatoa zawadi


Na Joyce Kasiki, Rukwa


BENKI ya CRDB imevutiwa na ubunifu unaofanywa na vijana wenye mahitaji maalumu wanaopata mafunzo katika vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), hatua iliyoifanya benki hiyo kuwapongeza, kuwazawadia na kuwafungulia akaunti za IMBEJU zinazolenga kuwawezesha kiuchumi.

Vijana hao wameonesha uwezo wa kutumia ujuzi walioupata kubuni vifaa mbalimbali vya kutatua changamoto za jamii, ikiwemo kifaa cha kuchaji  laptop (power bank), ushonaji huku ubunifu wao ukionesha fursa zilizopo kwa watu wenye ulemavu kujiajiri na kujitegemea.

Hatua hiyo imekuja wakati wa Wiki ya Vijana kitaifa inayofanyika Sumbawanga, mkoani Rukwa, ambapo CRDB imekuwa ikitoa elimu ya fedha na kutangaza huduma zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na watu wenye mahitaji maalumu kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa CRDB Tawi la Sumbawanga, Ruhore Masaka, amesema benki hiyo inatambua uwezo wa vijana wenye mahitaji maalumu na imejipanga kuhakikisha wanapata fursa sawa za huduma za kifedha bila kubaguliwa kwa misingi ya ulemavu.

Masaka amesema kupitia CRDB Foundation, benki hiyo ina programu ya akaunti ya IMBEJU inayolenga kuwasaidia vijana na wanawake kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, huku akaunti hiyo ikiwa na masharti yanayolenga kupunguza gharama za huduma za kibenki.

Amesema akaunti ya IMBEJU haina makato ya kila mwezi wala makato wakati wa kutoa fedha, na vijana wenye biashara au mawazo ya biashara wanaweza kuzingatiwa kwa ajili ya uwezeshaji wa mitaji kwa mujibu wa masharti ya programu hiyo.

Ameeleza kuwa lengo la benki hiyo ni kuwawezesha vijana, wakiwamo wenye mahitaji maalumu, kuendeleza bunifu zao na kuzigeuza kuwa fursa za biashara zitakazowaongezea kipato na kuwasaidia kujitegemea.

Kwa upande wake, Meneja wa Mahusiano na Taasisi za Serikali wa CRDB, Paskalina Diu, amesema benki hiyo inatumia Wiki ya Vijana kuwafikia vijana wa makundi mbalimbali kwa kuwapatia elimu ya fedha na kuwafahamisha kuhusu huduma zinazoweza kuwasaidia kufikia malengo yao.

Diu amesema CRDB inaamini kuwa vijana wanapaswa kupata fursa za kifedha bila kujali wanapoishi au changamoto wanazokabiliana nazo, wakiwamo vijana wenye mahitaji maalumu wanaotaka kuendeleza ujuzi na shughuli zao za uzalishaji.

Naye Francis Madanganya, mmoja wa wabunifu wenye mahitaji maalumu, ambaye amebuni kifaa cha kuchaji simu za mkononi (power bank), ameishukuru CRDB kwa kutambua juhudi zao na kuwaunga mkono katika kukuza ubunifu wao.

Madanganya amewahimiza vijana wenzake wenye ulemavu kutokata tamaa wala kujifungia nyumbani, badala yake wajitokeze kupata mafunzo katika vyuo vya VETA ambako wanaweza kujifunza fani mbalimbali zitakazowawezesha kutumia vipaji vyao kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.

Amesema mafunzo ya ufundi stadi yanaweza kuwapa vijana wenye mahitaji maalumu ujuzi wa kutengeneza bidhaa na kutoa huduma zinazohitajika katika jamii, hivyo kuwafungulia milango ya kujitegemea na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Kupitia hatua hizo, ushirikiano kati ya mafunzo ya ufundi stadi na upatikanaji wa huduma za kifedha unaonesha umuhimu wa kuwawezesha vijana wenye mahitaji maalumu kutumia ubunifu wao katika kujenga maisha bora na kushiriki katika uchumi wa nchi.