Na Penina Malundo,TimesMajira
MKUTANO wa 10 wa Baraza la Mawaziri la Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA) umekuwa fursa kwa nchi wanachama kutathmini utekelezaji wa maazimio ya mkutano uliopita uliofanyika Nairobi, Kenya, mwaka 2020 na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha usafiri wa majini, kukuza biashara na kuongeza ushiriki wa Waafrika katika sekta hiyo.
Akifungua mkutano huo leo jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha ushirikiano kwa kuunganisha miundombinu ya bandari, reli na barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa nchi wanachama.
Amesema maendeleo ya usafiri wa majini ni muhimu katika kuunganisha masoko na maeneo ya uzalishaji, akitaja Bandari ya Dar es Salaam kuwa lango muhimu la biashara linalohudumia Tanzania na nchi jirani.

Dkt. Nchemba amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji, ikiwemo reli ya kisasa ya SGR na ufufuaji wa reli ya TAZARA, ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutoka bandarini kwenda maeneo ya ndani na nchi jirani.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Tanzania itaweka msisitizo katika kuimarisha usafirishaji wa majini, kuongeza ushiriki wa nchi za Afrika katika umiliki na uendeshaji wa meli, kuendeleza wataalamu na kukuza uchumi wa buluu.

Naye Katibu Mkuu wa MOESNA, Kassim Mpaata, amesema takribani asilimia 88 ya biashara ya kimataifa husafirishwa kwa njia ya bahari, huku sehemu kubwa ya shughuli hizo ikidhibitiwa na kampuni za meli zinazomilikiwa na wageni.
Amesema hali hiyo inazifanya nchi za Afrika kulipa gharama za usafirishaji huku sehemu kubwa ya mapato ya sekta hiyo ikinufaisha wadau wa nje, akisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuunganisha rasilimali na kuongeza ushiriki wa Waafrika katika umiliki na uendeshaji wa meli.
Ameongeza kuwa mkutano huo unajadili itifaki ya kikanda ya usafirishaji wa mizigo na abiria kwa meli, ushirikiano baina ya kampuni za usafirishaji na maandalizi ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikanda cha Usafiri wa Majini kwa ajili ya elimu, utafiti na ubunifu.
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkoa huo una nafasi muhimu katika biashara na usafirishaji wa majini, akieleza matumaini kuwa maazimio yatakayofikiwa yatakuwa na manufaa kwa Watanzania na nchi nyingine wanachama.

More Stories
Mtandao walaani mauaji ya Wanawake, Wasichana nchini
UBA TANZANIA yazindua mfumo mpya wa malipo ‘PAPSS’
Ndejembi:Mradi wa TAZA kuchochea Maendeleo