Zitto achambua maeneo 10 ripoti ya CAG
Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewataka watu waache kumshauri Rais Samia Suluhu Hassan, kuacha kuendelea na miradi ya kimkakati iliyoachwa na Hayati Rais John Magufuli, bali anapaswa kuindeleza na kuboresha namna ya utekelezaji wake wa miradi hiyo.
Zitto alitoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusiana na hoja mbalimbali zilizoibuliwa kwenye Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020 iliyotolewa na CAG, Charles Kichere jijini Dodoma.
Amesema ni vema suala la kuachwa kwa miradi mbalimbali inayoachwa na marais wanaoondoka madarakani isijirudie, bali miradi hiyo iendelezwe, kwani kuiacha kutasababisha hasara kwa miradi ikiyokwisha anza kutekelezwa.
“Maoni yangu ni vema Rais Samia aiendeleze, tutafanya makosa makubwa tukiiacha, kwani huko nyuma tumeona hasara za kuacha miradi mikubwa,”amesema Zitto na kuongeza;
“Tayari tumeshawekeza pesa nyingi katika miradi mbalimbali mikubwa kama Mradi wa Stiegler’s Gorge, Mradi wa Reli na Ndege tukisema tuache hii ni hasara kubwa tutapata na hasara hiyo itaenda kwa nani? Jambo la kufanya ni kuhakikisha tunaboresha namna ya utekelezaji wa miradi na kupunguza madhara.”
Aidha amesema nchi isirudie makosa ya nyuma ya kila Rais mpya wanapoingia madarakani anakuja na miradi yake na kuacha ile iliyoanzishwa na mtangulizi wake.
“Tusimshauri Rais Samia kurudia haya ya nyuma, tuhakikishe tunamshauri kuendeleza miradi hii ikamilike, lakini ifanyiwe tathimini ni namna gani ya kuboreshwa utekelezaji wake ili iweze kuwa na tija,”amesema
Katika hilo la utekelezaji Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR), Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Mwalimu Julius Nyerere maarufu Stigler’s Gorge na ATCL, Zitto amesema Chama hicho kinamshauri Rais Samia, kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wake kujenga mifumo madhubuti ya Uwajibikaji na kuimarisha Taasisi za Uwajibikaji.
“Bila Taasisi imara nchi yetu haitaweza kupiga hatua kubwa za maendeleo, vinginevyo Miradi mikubwa kama Mradi wa Umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, Mradi wa Reli ya Kisasa na Mradi wa kufufua Shirika la Ndege la Taifa inaweza kugeuka kuwa miradi yenye hasara kubwa kwa Taifa iwapo hatua mahususi hazitachukuliwa kuingiza utaalamu, weledi na maarifa katika utekelezaji wake,” amesema Zitto
Ripoti ya CAG
Katika hatua nyingine, Zitto ametoa ushauri katika maeneo 10 ambapo chama hicho kinatoa mapendekezo ya kuchukuliwa kulingana na hoja zilizoibuliwa kwenye ripoti ya CAG.
Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa na CAG, Charles Kichere mwishoni mwa wiki, ilianisha madudu mbalimbali ya upigaji fedha za umma, yakihusisha wizara, mashirika ya umma.
Baadhi ya maeneo ambayo CAG alianisha upigaji wa fedha za umma ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), akaunti ya Zimamoto kupitisha malipo batili, hasara ya mabilioni ya fedha na ATCL kulemewa mzigo wa madeni pamoja na mikataba mibovu.
Kuhusu TPA
Kuhusu TPA, Zitto alishauri CAG afanye ukaguzi maalumu wa miradi yote mikubwa inayotekelezwa na TPA, Mamlaka ya Bandari ili kupata uhalisia wa ubadhirifu katika TPA.
“Wakati ukaguzi huo unafanyika tunapendekeza kuwa Mamlaka za Uteuzi zivunje Bodi ya Bandari na kuiunda upya ili kuweza kuweka misingi ya uwajibikaji katika Shirika,” amesema Zitto.
Anashauri madudu Mamlaka ya Bandari (TPA) yachunguzwe zaidi, hasa kwa kuzingatia kwamba Ripoti hii ya CAG imebaini vitendo vya ubadhirifu katika Bandari za Mwanza na Kigoma.
Hata hivyo, Zitto amesema hoja hiyo ya CAG ni sehemu ndogo sana ya ubadhirifu mkubwa ambao umekuwa ukifanyika katika Mamlaka ya Bandari Tanzania.
ATCL
Aidha, Zitto alishauri ufanyike ukaguzi wa ununuzi wa Ndege, kubadili muundo wa uendeshaji wa ATCL ili kupunguza hasara.
“Hoja ambayo imeleta mjadala mkubwa katika Ripoti ya CAG ni hasara kwa Shirika la Ndege la Taifa (ATCL). CAG alifanya ukaguzi wa kiutendaji (Startegic and Operational Efficiency) kwenye Kampuni ya Ndege Tanzania na kubaini kuwa Serikali ilikuwa imetumia sh. Trilioni 1.028 kununua Ndege ili kufufua Shirika la ATCL.
Kati ya Mwaka 2018/19 na 2019/2020 Mapato ghafi ya Shirika yaliongezeka kutoka sh. 112 bilioni kwa mwaka mpaka sh. 158 bilioni kwa mwaka sawa na ongezeko la asilimia 41.
Katika kipindi hicho pia Matumizi ya Shirika yaliongezeka kwa asilimia 45 kutoka sh. bilioni 134 mpaka sh, bilioni 193. Pamoja na kununua ndege, kwa miaka mitano yaani kuanzia 2015/16 hadi 2019/20 Serikali imeisaidia Kampuni ya Ndege kiasi cha Sh. Bilioni 153.711 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na maendeleo.
Fedha hizi za Walipakodi Serikali imekuwa ikizitoa kama ruzuku kwa ATCL.
Hata hivyo Shirika limekuwa na hasara ya jumla ya sh. bilioni 153 katika miaka mitano ikiwemo hasara ya sh. bilioni 60.25 mwaka 2019/2020. Ruzuku yote ambayo Serikali imekuwa inadumbukiza ATCL imeliwa na hasara.
“Hata hivyo, Zitto alihoji ilikuwaje CAG hakueleza katika Ripoti yake ilikuwaje Shirika ambalo lina hasara kiasi hicho licha ya Ruzuku ya Serikali liliweza kulipa Gawio kwa Serikali,” amesema Zitto.
Zitto, alishauri CAG afanye ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma sh. Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege.
“Afanye ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa Ndege za Serikali na Shirika la Ndege la ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya fedha zao za kodi,” amesema Zitto.
“Tunapendekeza kuwa CAG afanye ukaguzi wa manunuzi ya Ndege ili tuweze kujiridhisha kama taratibu zote za manunuzi zilifuatwa na nchi kupata thamani ya fedha,” amesema..
Amesema pamoja na hasara iliyobainishwa na CAG kuna matumaini makubwa katika Shirika la ATCL. “Kinachohitajika ni maamuzi sahihi yenye maarifa ya sekta husika,” amesema Zito.
Alipendekeza muundo wa umiliki wa ATCL ubadilishwe kwa kuhusisha mashirika ya uhifadhi na utalii kama wamiliki. “Shirika la TANAPA na NCAA wamilikishwe asilimia 60 ya Kampuni na hivyo waondolewe katika orodha ya Mashirika ya kupeleka Hazina asilimia 15 ya Makusanyo yao ghafi,” amesema Zitto.
Aidha, alipendekeza mashirika haya ya Utalii yaachiwe kujiendesha na kukusanya mapato yao wenyewe, asilimia 40 zilizobakia zimilikiwe na Serikali ambapo Kampuni ikikaa vema asilimia 25 ya Shirika wamilikishwe wananchi kwa kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kuongeza uwazi na kuboresha misingi bora ya uendeshaji wa Kampuni .
Deni la MSD
Katika hatua nyingine Zitto amesema chama hicho kinapendekeza Serikali ilipe Deni lote la MSD, na pia Serikali itoe mtaji kamilifu kwa MSD ili iweze kujitegemea kibiashara katika shughuli ya usambazaji wa dawa kwa wananchi wetu.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini