Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Othman alitoa kauli hiyo leo Julai 12, 2026, alipokuwa akizungumza na viongozi wa chama kutoka ngazi mbalimbali katika kikao cha ndani kilichofanyika Ukumbi wa PICCA DILY, Nyamazi, Mkoa wa Mjinii Unguja. Alieleza kuwa kikao hicho kilifanyika ndani badala ya mkutano wa hadhara uliokuwa umepangwa kufuatia agizo la Waziri wa Mambo ya Ndani kuzuia mikutano hiyo.
“Huyu Waziri wa Mambo ya Ndani atambue kuwa anakosea anapoogopa watengeneza amani,” amesema Othman.
Amefafanua kuwa ni sahihi viongozi kuwa na tahadhari dhidi ya vurugu, lakini si sahihi kuwaogopa watu wanaohamasisha amani na mazungumzo ya kisiasa.
“Unapopambana anayetengeneza amani, unaonyesha kuendesha mambo ya nchi kwa kubahatisha. Nchi haiendeshwi kwa kubahatisha; inaongozwa kwa sheria na taratibu ambazo zinapaswa kutumika kwa usawa, si kwa matakwa ya mtu mmoja,” amesema.
Akionesha kitabu cha sheria za Zanzibar za miaka ya nyuma, Othman amesema Zanzibar ina historia ndefu ya kuongozwa kwa misingi ya sheria. Alibainisha kuwa sheria inayosimamia Jeshi la Polisi Zanzibar ilitungwa mwaka 1899, sheria ya kudhibiti vibaka mwaka 1905, na sheria ya kulinda haki za wanyama mwaka 1918.
Amesisitiza kuwa pamoja na kuwapo kwa Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 iliyounganisha mfumo wa usajili wa vyama nchini, Zanzibar bado ina utamaduni na utaratibu wake wa kufanya siasa ambao unapaswa kuheshimiwa.

Akizungumzia mazungumzo kati ya ACT Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhusu kuondoa mkwamo wa kisiasa Zanzibar, Othman alisema pande hizo zimekubaliana katika maeneo kadhaa muhimu ya mageuzi.
Ametaja miongoni mwa makubaliano hayo kuwa ni kupitia upya Katiba ya Zanzibar, kufanya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi kuanzia Tume ya Uchaguzi, sekretarieti na watendaji wake, kuondoa mfumo wa kura ya mapema, kuimarisha mfumo wa Serikali za Mitaa na kupitia upya suala la Kitambulisho cha Mzanzibari.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa, amesema Zanzibar imevuka salama matukio ya Oktoba 28 na 29, 2025 kutokana na busara na uongozi wa Mwenyekiti wa Taifa, Othman Masoud Othman.
Amesema viongozi wa ACT Wazalendo ni wastaarabu na wako tayari kutekeleza kwa vitendo makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande mbili.
“Sisi ni wastaarabu, na kwa upande wetu tuko tayari kuyatekeleza yote tuliyokubaliana. Tutatangulia mbele katika utekelezaji wake,” amesema Jussa.
Naye Mwenyekiti Mstaafu wa ACT Wazalendo, Juma Duni Haji, amesema ana imani makubaliano hayo yatafanikiwa na kuimarisha umoja wa Wazanzibari.
Amewataka wananchi wenye wasiwasi kuhusu utekelezaji wa makubaliano hayo kuwa na matumaini, akisisitiza kuwa yaliyokubaliwa yatatekelezwa kwa wakati.
“Sisi hatuwezi kukubali jamii yetu ivurugwe makusudi,” amesema Duni.
Aidha, ameshauri kuandaliwa kwa nyaraka maalumu zitakazogawiwa kwa wananchi ili kila mmoja afahamu kwa undani yaliyokubaliwa katika mazungumzo hayo.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Is-haka Rashid Mchinjita, amewataka Wazanzibari kupuuza wanaopinga maridhiano hayo, akisema juhudi za kuleta umoja zinapaswa kuungwa mkono.
“Ukimuona mtu anapinga juhudi za kuleta umoja, huyo hafai katika jamii yetu,” amesema.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe, alisema kufikiwa kwa makubaliano hayo kunaonesha umakini wa viongozi wa chama chao katika kusimamia mazungumzo yenye lengo la kuimarisha umoja wa Wazanzibari.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa wa ACT Wazalendo upande wa Unguja, Mansour Yusouf Himid, amesema lengo la Mapinduzi ni kuimarisha umoja wa wananchi na si kuwagawa.
“Utamaduni wetu ni kuwa wamoja na kufanya kazi pamoja. Hiyo ndiyo desturi yetu,” amesema Mansour.
Amempongeza Mwenyekiti wa Taifa, Othman Masoud Othman, kwa uongozi wake na kusimamia haki za wananchi, akisema uongozi wake umeendelea kuwapa matumaini Wazanzibari katika kuendeleza mapambano ya kudai haki na maridhiano.

More Stories
Wananchi waendelea kunufaika na Ofa za TTCL Sabasaba
Prof. Rasheli apongeza shughuli za REA Sabasaba 2026
Wizara yasuluhisha mgogoro wa Kampuni na Mkandarasi