Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema chama hicho kimeingia kwenye mazungumzo ya kisiasa kwa lengo la kulinda amani ya kweli na maslahi ya wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza Pandani wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Kikatiba wa jimbo hilo, Othman alisisitiza kuwa uamuzi wa kushiriki mazungumzo haukulenga maslahi ya vyama vya siasa bali wananchi.
“Licha ya yote yaliyotokea, tulikubali kukaa kwenye meza kwa maslahi ya Wazanzibari na si ya vyama vyetu,”amesema.
Ameeleza kuwa mazungumzo hayo yanalenga kurejesha mamlaka ya nchi mikononi mwa wananchi, akibainisha kuwa hatua zilizofikiwa zinaungwa mkono na wengi kwa lengo la kuimarisha umoja wa kitaifa.
“Nakuambieni ukweli, tumefikia pahala ambapo tumekubaliana na wengi wanaunga mkono ili nchi iwe na umoja, na Insha Allah tutafikia,” ameongeza.

Aidha, amewataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kuendelea kudumisha umoja, akisisitiza kuwa huo ndiyo msingi wa mapambano yao ya kisiasa.
Othman amefafanua kuwa ACT Wazalendo si chama cha kutafuta ushindi wa uchaguzi pekee, bali kinahimiza ukombozi wa nchi na uendeshaji wa dola kwa misingi ya ustaarabu na maadili.
Katika kuimarisha chama, amewahimiza viongozi na wanachama kutimiza wajibu wao, kufanya tathmini ya utendaji, pamoja na kuimarisha matawi ambayo ndiyo msingi wa chama.

“Chama chetu si SACCOs, bali ni chama kinachoendesha shughuli zake kwa nguvu za wanachama wake, si kwa kutegemea dola,” amesisitiza.
Pia amewataka viongozi kuwa karibu na jamii na kushughulikia kero za wananchi kama sehemu ya kukuza maendeleo ya kisiasa.“Chama chetu ni kikubwa, lazima tuwe karibu na jamii katika mazingira mbalimbali,” amesema Othman, maarufu kama OMO.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amekabidhi gari moja kati ya manne yaliyotolewa kwa pamoja na Mbunge Muhammed Khalfan pamoja na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Profesa Omar Fakih Hamad wa Jimbo la Pandani, kwa ajili ya huduma za kijamii katika shehia zote nne za jimbo hilo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar wa chama hicho, Omar Ali Shehe, amesisitiza kuwa uimara wa majimbo na matawi ndiyo nguzo kuu ya chama, akihimiza maeneo mengine kuendeleza mikutano mikuu ya kikatiba.
“Mikutano kama hii inaonyesha uimara wa chama chetu na uwepo wa viongozi madhubuti,” amesema.
Naibu huyoNaye Mwenyekiti wa Mkoa wa Wete kichama, Juma Khamis Ali, aliwataka wanachama kuimarisha mshikamano na ushirikiano ili kufikia malengo ya chama hicho.
Mkutano huo umeashiria kuanza rasmi kwa mikutano ya majimbo ya ACT Wazalendo kote Tanzania.

More Stories
Watumishi NIRC washerehekea mwaka 2026,waaswa kuimarisha mshikamo,uwajibikaji
Wanaume Summit 2026 kukutanisha washiriki zaidi ya 2,000
Chongolo, azindua kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”