March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Nchimbi kuunguruma Pemba leo

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Pemba

MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel Nchimbi, amewasili Mkoa wa Kusini Pemba, kuendelea na kampeni ya kukinadi chama hicho na kuwaombe kura wagombea wa CCM,katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

Dkt. Nchimbi alimaliza kampeni mkoani Tabora Oktoba 06, 2025 na sasa yupo Pemba, ambapo akiwa mkoani Tabora alifanya mikutano kadhaa akieleza mafanikio yaliyopatikana kipindi cha uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na matarajio na mikakati itakayotekelezwa katika kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.

Akiwa Tabora, baadhi ya ahadi alizotoa kwa wakazi wa mkoa huo Dkt. Nchimbi ni pamoja na CCM imedhamiria kuendelea kuleta miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali katika sekta ya elimu, afya, kilimo, miundombinu ya barabara.

Huku kwa upande wa Tabora kurejesha viwanda vya kuchakata tumbaku,kusimamia na kulinda haki za wakulima wa tumbaku na mazao mengine.

Pia amesema, Serikali ya CCM itasimamia kwa ukaribu mpango bora wa matumizi ya ardhi ili kuziwezesha jamii za wakulima na wafugaji kuendesha shughuli zao bila migongano, kujenga masoko ya kisasa na minada yenye hadhi pamoja na kusambaza maji katika vijiji na vitongoji.

Leo akiwa Pemba , Dkt. Nchimbi anaanza na mkutano utakaofanyika eneo la Kinyasini Wilaya ya Wete na baadae atahitimisha kampeni Zanzibar kwa mkutano mkubwa huko Kusini Unguja Jimbo la Chwaka.