

Na Joyce Kasiki, TimesMajura Online – Geita
MWENYEKITI wa Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Geita, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa Mstaafu wa mkoa huo Mhandisi Robert Gabriel ameupongeza Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuwekeza katika kiwanda cha kutengeneza viatu vya ngozi, kinachojulikana kama Kilimanjaro International Leather Industries, ambacho kimeleta bidhaa bora sokoni zenye viwango vya kimataifa.
Mhandisi Gabriel ametoa pongezi hizo alipotembelea banda la PSSSF katika maonyesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini katika viwanja vya Dkt.Samia Suluhu Hassan Bombambili mkoani Geita.
“Wale waliokuwa wakisema kiwanda cha viatu cha Bora kilikufa, sasa ni mashahidi wa kuibuka kwa bidhaa bora kabisa. Viatu vyao ni imara, ni vya ngozi safi na vinapatikana hapa hapa nchini. Wazazi wanaojali watoto wao wanapaswa kuvitafuta,” amesema.
Amewataka wafanyabiashara na Watanzania kwa ujumla kuunga mkono viwanda vya ndani kwa kununua bidhaa za viatu pamoja na bidhaa nyingine nyingi kutoka kiwanda hicho badala ya kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi.
“Ukiwa unavaa kiatu cha Tanzania, siyo tu unasaidia ajira, bali pia unalipa kodi na unaiinua familia ya Mtanzania. Huu ndiyo uzalendo wa kweli. Tanzania ya viwanda si hadithi tena,” amesisitiza.
Pia, Mhandisi Gabriel aliitaja PSSSF kama mfano wa mafanikio kwa kuwekeza katika Kiwanda cha Kusindika Nyama ambacho kinazalisha nyama laini ya kiwango cha kimataifa inayopakiwa kitaalamu kwa ajili ya masoko ya ndani na nje ya nchi ikiwemo Asia, Qatar, na Saudi Arabia.
“Tulizoa kununua nyama za ng’ombe waliovurugwa ,nyama yao inakuwa ngumu,lakini sasa, Tanzania tuna nyama laini, bora ya kisasa,kiwanda chetu kinanunua ng’ombe, kinawanenepesha, kinachinja kwa viwango, kinapaki vizuri,hii ni hatua kubwa sana,” alieleza.
Amesisitiza kuwa kama Chemba, wako tayari kuwaunganisha wabunifu na wajasiriamali wenye miradi ya kiuchumi ili kupata ushauri na fursa za kushiriki katika miradi inayochochea uchumi wa Taifa.
Mhandisi Gabriel ambaye ni mwanzilishi wa maonyesho hayo,ametumia nafasi hiyo kuongeza juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza Maonyesho ya Madini Geita hadi kufikia hatua ya kuwa na majengo ya kudumu ya taasisi mbalimbali.
Aidha, alitaja uwepo wa wageni kutoka nje ya nchi kama Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, DRC na Kenya kuwa ishara ya hadhi kubwa ya maonyesho hayo.
“Kama Chemba, tunawakilisha makundi yote ya kibiashara. Tumeamua kutoa shukrani kwa mafanikio yaliyopatikana, lakini pia kueleza changamoto tunazokutana nazo ili zitatuliwe kwa pamoja,” amesema Mhandisi Gabriel.
Afisa Mauzo Mwandamizi wa Kiwanda cha Kilimanjaro International Leather Christopher Manyani,amesema bidhaa za kiwanda hicho ni za hali ya juu na hutengenezwa kwa kutumia ngozi ya wanyama kutoka Tanzania.
“Bei ya viatu inategemea na aina ya kiatu, lakini ni nafuu kuliko ya nje. Wananchi na wafanyabiashara waje waone na wanunue viatu vyetu bora vya ndani,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Noel Tuga, Afisa Mwandamizi wa Uwekezaji kutoka PSSSF, ameeleza kuwa miradi ya nyama na viatu ni sehemu ya mikakati ya mfuko huo katika kuchochea uchumi wa ndani na kutoa ajira kwa Watanzania.
“Tunaamini Tanzania imefunguka. Viwanda vipo. Tunahamasisha wananchi waunge mkono bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kuongeza tija na kuinua uchumi wa nchi,” amesema Tuga.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi