March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Tulia:Siku 100 za Rais Samia zitaleta bima ya afya kwa familia zisizojiweza

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

SPIKA wa Bunge na Mgombea Ubunge wa Jimbo jipya la Uyole kupitia CCM,Dkt.Tulia Ackson, amesema kuwa ndani ya siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, familia zote zisizojiweza zitapatiwa bima ya afya, ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote iliyopitishwa bungeni.

Dkt.Tulia ameitoa kauli hiyo Septemba 27 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Tembela, ulioshirikisha viongozi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini na machifu.

“Kwenye eneo la afya, tumekuwa tukiendelea kuwapatia bima familia zisizojiweza kwa jitihada za Mbunge, lakini sasa kupitia Rais Samia zoezi hili litafika familia zote maskini,” amesema Dkt. Tulia.

Aidha, ameibainisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimejipanga kuwatumikia wananchi wa Uyole katika nyanja za afya, elimu, umeme, maji, barabara na huduma nyingine muhimu.

Kwa upande wake, Diwani Mteule wa CCM kata ya Tembela, Frank Mwasyoke, amesema kipaumbele chao ni kuboresha zahanati ya kata hiyo ili iwe kituo cha afya.

“Tunajua hili siyo jambo kubwa kwako Mheshimiwa Tulia. Ukiwa Mbunge wa Jimbo la Mbeya uliweza kusimamia kata 36, leo una kata 13 pekee tunaamini hili kwetu Tembela litaisha,” amesema Mwasyoke.

Naye mmoja wa wananchi, Joseph Anangisye, amesema changamoto kubwa katika eneo hilo ni barabara na maji, lakini anaamini zitapatiwa suluhu kupitia uongozi wa Dkt. Tulia.