WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Mhifadhi Mwandamizi Juma Mdoe, wameungana na wadau wa sekta ya madini kwa kushiriki kwenye Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika mkoani Geita ili kutoa elimu kwa wadau hao ya namna ya karudisha uoto wa miti wanayoikata wakati wa utafutaji na uchimbaji wa madini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho hayo, Mhifadhi Mwandamizi Mdoe amesema kuwa wachimbaji wa madini ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa rasilimali za misitu, hasa miti, hivyo ni muhimu wakahusishwa moja kwa moja katika juhudi za kuhifadhi mazingira.
“Shughuli za uchimbaji zinahitaji matumizi makubwa ya miti hasa katika kutengeneza maboksi yanayowekwa migodini kuzuia udongo usiporomoke. Tunawasisitiza wadau hawa kutambua kuwa wanalo deni la kurejesha uoto wa asili kwa kupanda miti baada ya matumizi,” amesema Mdoe.
Ameongeza kuwa lengo kuu la ushiriki wao katika maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wachimbaji na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu na mazingira.
Ameeleza kuwa TFS inahamasisha matumizi endelevu ya misitu ili jamii iendelee kunufaika kwa muda mrefu kupitia huduma za kiikolojia kama vile upatikanaji wa hewa safi,vyanzo vya maji safi,samani na mazao ya misitu,ufugaji wa nyuki na kipato chake na utalii wa ikolojia na wanyamapori
Katika kuonyesha fursa zilizopo kwenye uhifadhi, Mdoe alitaja baadhi ya hifadhi na mashamba ya miti yanayosimamiwa na TFS ambayo yana faida nyingi kiikolojia na kiuchumi. Hifadhi hizo ni pamoja na Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Kome Sengerema, shamba la miti Silayo linatoa fursa za utalii, nyuki, na uoto wa asili,shamba la miti Lubari – Kagera, lenye maporomoko ya maji.
Pia amesema kuna Hifadhi za Amani, Magamba, Minziro na nyingine zinazotoa fursa za utalii wa picha na wanyama adimu
Kwa upande mwingine amesema, TFS imeendelea kutoa elimu na vibali kwa wananchi wanaotaka kufanya ufugaji wa nyuki katika hifadhi au mashamba ya miti.
“Kwa wale wanaohitaji maeneo ya kufugia nyuki, tunawapatia vibali rasmi ili waingize mizinga yao kwa utaratibu unaozingatia uhifadhi,” amesema Mdoe.
Aidha, TFS inatoa mafunzo mbalimbali ya kitaalamu kuhusu tabia na maisha ya nyuki,njia za kujikinga na nyuki,umuhimu wa bidhaa za nyuki kama asali na sumu ya nyuki.
Akifafanua kuhusu faida za kiafya, Mdoe ameeleza kuwa sumu ya nyuki ina uwezo mkubwa wa kudhibiti bakteria, fangasi, na virusi, huku ikisaidia mwili wa binadamu kujenga kinga dhidi ya magonjwa na kusaidia kupunguza vimbeKwa kumalizia, Mhifadhi huyo amehimiza jamii inayozunguka hifadhi za misitu kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi, akisisitiza kuwa misitu ni urithi wa taifa unaopaswa kulindwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi