Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Tanganyika.
CHANGAMOTO ya barabara zisizopitika umefikia kikomo katika Kijiji cha Milala Kata ya Tongwe Wilaya ya Tanganyika Mkoani Katavi, baada ya Wakala ya Barabara Vijiji na Mjini TARURA kukamilisha ujezi wa barabara za kilometa nne za kiwango cha lami.
Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hizo umetajwa kuwa kiungo muhimu kwa wasafiri na wasafirishaji wa bidhaa, mazao na malighafi mbalimbali kutoka mashambani, sokoni na wakati wa kwenda kutafuta huduma za kijamii kama vile hosptalini na shuleni kwa wanafunzi.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Tanganyika Mhandisi Nolasco Kamasho, akisoma taarifa kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ussi alisema ujenzi wa barabara hizo za Mji wa Majalila zenye urefu wa kilometa nne kwa kiwango cha lami zimegharimu shilingi bilioni 1,862, 544,675 kwenye ujezi huo.
Mha.Kamasho akiwa katika eneo la uzinduzi wa barabara hizo katika Kijiji cha Majalila alisema utekelezaji wa ujenzi barabara unatokana na fedha za road fund, hivyo kama TARURA walikuwa na jukumu la kuhakikisha ujenzi wa barabara unakamilika kwa wakati huku ukiendana na thamani halisi ya fedha.
“Barabara hizi zitakuwa chachu ya ustawi wa maendeleo ya watu kiuchumi” Alisema Meneja huyo akiwaomba wananchi kulinda miundombinu ya barabara hiyo isiharibiwe kwani inatumia fedha nyingi.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ussi, baada ya kuzindua barabara hizo licha ya kuipongeza TARURA kwa kazi nzuri ya kusimamia ujenzi wa barabara hizo vilevile alisema utekelezaji makini wa majukumu ya TARURA utawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi.
Alisema kujikwamua kiuchumi ni kutokana na unafuu utakaokuwepo kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji hivyo kila mmoja atanufaika na ukuaji wa uchumi.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko, akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Kigoma alisema Mbio za Mwenge wa Uhuru zikiwa mkoani humo utatembelea miradi 46 yenye thamani zaidi ya bilioni 10.
Ambapo katika wilaya ya Tanganyika Mwenge wa Uhuru pia umezindua,Mradi wa maji Mazwe wenye thamani shilingi 307, 675,300/=, mradi wa zahanati Kijiji cha Vikonge wenye thamani ya shilingi 214, 239,749/=, mradi wa bweni la wasichana shule ya sekondari Majalila wenye thamani ya shilingi 173, 314, 000/=, Ugawaji wa mitungi ya gesi 20 yenye thamani ya shilingi 1,000,000/=, na kutembelea mradi wa vijana wa kikundi cha Bodaboda na Samia Ifukutwa yenye thamani ya shilingi 19,121,745/=
Mkazi wa Kijiji cha Majalila Maria Shija ameishukuru serikali ya awamu ya sita ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ya kuwajengea miundombinu wezeshi itakayowasaidia kupata mafanikio ya kimaendeleo.
Maria alisema kukamilika kwa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami utawasaidia kufika kwa wakati katika huduma za kijamii kama vile katika vituo vya afya na kuondoa adha ya wasafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali kutoka kwenye soko au kupeleka kwenye soko.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi