March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi wajitokeza kujisajili BRELA maonyesho ya Madini

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Geita

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) unashiriki kikamilifu katika Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika kwenye viwanja vya Dkt.Samia Suluhu, mkoani Geita, kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali za usajili na utoaji wa leseni kwa wananchi na wawekezaji.

Akizungumza katika viwanja vya maonyesho hayo katika banda lao,Kaimu Meneja wa Leseni za Viwanda kutoka BRELA, Bw. Yusuph Nakapala amesema BRELA inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi na kuhakikisha kila mfanyabiashara anatimiza matakwa ya kisheria kuhusu usajili na uwasilishaji wa taarifa muhimu za kibiashara.

Amesema,taasisi hiyo inatoa huduma zote muhimu kwa wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda ikiwemo usajili wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na huduma, usajili wa hataza, pamoja na utoaji wa leseni za kundi “A” na vyeti vya usajili.

“Tunatoa pia huduma za baada ya usajili kama vile uwasilishaji wa mizania ya mwaka kwa kampuni, taarifa za maendeleo ya viwanda kwa wamiliki wa viwanda, pamoja na taarifa za wamiliki wa manufaa (beneficial owners). “Amesema Nakapala

Aidha amewahimiza wananchi wa Geita na maeneo jirani kufika kwenye banda la BRELA ili kupata huduma hizo muhimu.

Ameeleza kuwa, mwanzoni mwa maonesho, mwitikio ulikuwa mdogo, lakini kwa sasa wananchi wameanza kujitokeza kwa wingi na wamekuwa wakisaidiwa kutatua changamoto walizokuwa nazo.

Ameongeza kuwa BRELA imeboresha mifumo yake ya utoaji huduma kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo hata nje ya Geita.

“Huduma zetu zinapatikana popote ulipo kupitia mifumo ya kidijitali. Tumejipanga kuhakikisha mteja wetu hapati usumbufu awe Geita au mkoa mwingine, bado anaweza kupata huduma zetu kwa urahisi,” ameongeza.

Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la BRELA wametoa maoni chanya kuhusu huduma zinazotolewa huku wakipongeza huduma hiyo kuwepo katika maonyesho hayo.

Bw. Kiliamu Simiozi, ambaye anatoka ofisi ya Mtemi Able, amesema alikuja kupata huduma ya kusajili na kurekebisha taarifa za biashara na ameridhishwa na lugha rafiki na ufanisi wa watumishi wa BRELA.

“Huduma ni nzuri sana. Ukifika hapa unaweza kukamilisha nyaraka zako na kuondoka nazo siku hiyo hiyo bila kusubiri. Natoa wito kwa ndugu zangu ambao hawajafanya usajili kufika na kupata huduma hizi,” amesema Bw. Simiozi.

Naye Bw. Zedekia Gabriel, ambaye alifika kwa ajili ya huduma ya usajili wa Beneficial Owner, amesema awali ombi lake lilichukua muda mrefu katika mfumo, lakini sasa limepatiwa suluhisho. Ameeleza kuwa kila kampuni inapaswa kuwasilisha taarifa za mmiliki wa manufaa kama sheria inavyoelekeza.